WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imeweza
kutoa mafunzo kwa vijana 11,492 katika fani
mbalimbali kupitia vyuo vya umma, binafsi na makampuni ikiwa ni utekelezaji wa Programu
ya Taifa ya Miaka Mitano ya Kukuza Ujuzi.
Amesema programu hiyo ambayo ilianza kutekelezwa katika mwaka wa fedha
2016/17, inalenga kuweka maeneo mahususi ya kuwezesha vijana wawe na ujuzi
stahiki wa kuajirika au kujiajiri katika soko la ajira la ndani na la nje ya
nchi.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Ijumaa, Novemba 17,
2017) bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja ya
kuahirisha mkutano wa tisa wa Bunge la 11. Bunge limeahirishwa hadi Januari 30,
mwakani.
Amesema katika kutekeleza programu hiyo, Serikali
imejikita katika maeneo ya kutoa mafunzo ya kukuza ujuzi kwa njia ya uanagenzi
(apprenticeship); kutoa mafunzo ya
ujuzi na uzoefu kazini (internship)
kwa wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu na mafunzo hususan wale wa vyuo vikuu;
kutoa mafunzo ya urasimishaji ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa mafunzo;
na kutoa mafunzo ya kukuza ujuzi kwa walio makazini.
Waziri Mkuu amesema katika kujenga ujuzi wa vijana kushiriki kwenye
shughuli za kilimo, Serikali imeandaa mafunzo maalum ambayo yataanza rasmi
Desemba, 2017 katika Halmashauri zote zilizowasilisha maombi.
“Tumeshirikisha Wakuu wa Mikoa yote na kuwaelekeza waandae maeneo ya
kujifunzia vijana hao kwenye Halmashauri zote za mikoa yao,” amesema.
Amesema ofisi yake imepokea
maombi ya kushiriki kutekeleza programu ya kukuza ujuzi katika eneo la kilimo
kwa kutumia teknolojia ya kitalu nyumba (Green House) kutoka mikoa
mitano ya Kagera, Manyara, Ruvuma, Kilimanjaro na Shinyanga. “Ofisi yangu
imefika katika Halmashauri zote za mikoa hii ili kujiridhisha kuwa imetenga maeneo
kwa ajili ya kujenga vitalu vyumba vya kufundishia,” ameongeza.
Amesema katika mwaka huu wa fedha (2017/18), Serikali kwa kushirikiana na
sekta binafsi imetoa fursa za mafunzo mbalimbali ya vitendo kupitia Chama cha
Waajiri Tanzania (ATE), Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) na Baraza la
Taifa la Biashara (TNBC) na kukubaliana kuwa ifikapo Desemba, 2017 vijana wote wawe
wamepatiwa fursa za mafunzo katika maeneo ya kazi.
Waziri Mkuu ametoa wito kwa viwanda na taasisi mbalimbali zishirikiane na
Serikali kuwapa nafasi kwa vijana ili wajifunze kwa vitendo katika maeneo ya
kazi na kupata uzoefu na ujuzi stahiki.
“Tuna vijana wengi waliomaliza vyuo vikuu walioomba kushiriki mafunzo ya
vitendo na kupata uzoefu wa kazi. Natoa wito kwa waajiri watoe nafasi kwa
vijana wetu hawa kujifunza kwa vitendo. Serikali itaendelea kugharamia mahitaji
ya msingi ya vijana hawa wakati wa mafunzo hayo,” amesisitiza.
No comments:
Post a Comment