HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 10, 2017

WAZIRI JAFO: NINA IMANI NA MAAFISA MAENDELEO YA JAMII KATIKA KUJENGA UCHUMI WA VIWANDA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo akizungumza na Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka katika Mikoa na Halmashauri nchini na kusisitiza kuwa ana imani nao katika kujenga uchumi wa Viwanda wakati akifunga Mkutano Mkuu wa 12 kwa Wataalm wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii uliofanyika kwa siku nne katika Ukumbi wa Chuo cha Mioango Dodoma. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW).

Na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mhe. Selemani Jafo ameeleza imani yake kubwa kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii katika kuamsha ari ya wananchi kushiriki katika shughuli za Maendeleo zitakazowezesha kufikia uchumi wa viwanda.


Ameyasema hayo Mjini Dodoma wakati akifunga Mkutano wa 12 wa Wataalam wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii uliofanyika kwa siku nne katika Ukumbi wa Chuo cha Mipango.


Mhe. Jafo ameeleza kuwa kama Maafisa Maendeleo ya Jamii wakitumika vizuri katika maeneo yao wataleta mabadiliko yenye tija yatakayosaidia kufikia uchumi wa viwanda.


“ Nina imani na Maafisa Maendeleo ya Jamii katika kutumia weledi walionao kufanikisha kampeni ya kitaifa ya viwanda vyetu, mkoa wetu ambayo nimeizindua hapa mkoani Dodoma” alisema Mhe. Jafo.


Mhe Jafo amefafanua kuwa Kampeni hii imeanzishwa kwa lengo la kusisimua na uanzishaji wa angalau viwanda 100 kwa kila mkoa ndani ya jamii ya Tanzania ambao utasimamiwa na Maafisa Maendeleo ya Jamii katika kuamsha ari na kuipa kipaumbele katika utendaji wao wa kila siku.


Ameongeza kuwa watanzania wanamatarajio makubwa na Serikali ya Awamu ya Tano ya kuwa na Tanzania ya viwanda na azma hiyo itaweza kufikiwa kupitia kwa Maafisa ya Maendeleo ya Jamii ambao ni mawakala wa mabadiliko katika jamii zetu.


Mhe. Jafo amesisitiza kuthamini kada ya Maendeleo ya Jamii na kuwaagiza wakurugenzi wa Halmashauri ambao walishindwa kuleta watumishi wao kwenye mkutano mkuu wa mwaka wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii kujieleza kwake na watakuwa na jukumu la kutoa taarifa ya kazi zilizofanyika chini ya utendaji wa Idara ya Maendeleo ya Jamii.


Kwa upande wake Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bibi. Sihaba Nkinga amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii kwenda kufanya kazi kwa hamasa kubwa ili kuacha alama katika jamii kwa kuonesha matokeo mazuri ya kazi zilizofanyika wakati wa utumishi wao kwa umma.


Mkutano Mkuu wa mwaka wa Wataalam wa Maendeleo ya Jamii umemalizika Mjini Dodoma na kutoka na maazimio muhimu yakiwemo kwenda kuleta mabadiliko kwa wananchi kwa kuamsha ari yao ya kujishughulisha katika kujiletea Maendeleo yao na taifa kwa ujumla ili kuwezesha kufikia uchumi wa viwanda.

No comments:

Post a Comment

Pages