HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 16, 2017

KUWEIT KUIUNGA MKONO SMZ KATIKA MIRADI YA MAENDELEO

Serikali ya Kuweit imeihakikishia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuendelea kuiunga mkono katika harakati zake za kuimarisha ustawi wa Wananchi wake pamoja na miradi ya maendeleo.

Hatua hiyo itakwenda sambamba na Mpango Maalum uliobuniwa na Ofisi ya Ubalozi wa Kuweit Nchini Tanzania katika kusaidia Vifaa pamoja na zana za Kisasa zitakazowawezesha Watu wenye ulemavu kutengeneza vitu vya sanaa katika kiwango cha Kitaalamu.

Balozi wa Kuweit Nchini Tanzania Bwana Jassem Al – Najem alitoa kauli hiyo wakati akikabidhi zawadi ya Vifaa vya Viti, Magongo, Miwani Pamoja na Mbao za kusomea kwa ajili ya Wananchi wenye mahitaji maalum Zanzibar hapo Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Vuga Mjini Zanzibar.

Zawadi hizo alizokabidhiwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi imegharimu Dola za Kimarekani Laki Tano sawa na shilingi za Kitanzania Bilioni 1.1.

Balozi Jassem alisema jitihada zinazochukuliwa na Kuweit katika kusaidia huduma za Kijamii katika Mataifa Rafiki yale yenye mahitaji maalum alizieleza kuwa zitakuwa endelevu.

Balozi wa Kuweit Nchini Tanzania kupitia shughuli hiyo maalum alitoa mkono wa pole kwa Wanzania na Watanzani wote kufuatia vifo vya Askari 14 wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania { jwtz} waliouawa huko DRC.

Balozi Jassem alisema kitendo kilichofanywa na waasi wa ADF hakikubaliki kabisa Kimataifa kwa vile kimekwenda kinyume na sheria na taratibu zilizowekwa na Umoja wa Amani katika maeneo yanayopatiwa ulinzi wa amani.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kufuatia zawadi hiyo ya Serikali ya Kuweit Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Vifaa hivyo ni mkombozi mkubwa kwa Watu wenye Ulemavu hapa Zanzibar.

Balozi Seif alisema Watu wenye ulemavu hawakujitakia kuwa na maumbile waliyokuwa nayo bali ni kudra tuu za Mwenyezi Muungu ambazo wanapaswa kuendana nazo katika misingi na utaratibu wa ustahamilivu.

Alisema Jamii inapaswa kutambua kuwa na wao ni walemavu watarajiwa. Hivyo alisisitiza umuhimu wa Wananchi kuendelea kuwaenzi na kuwatunza Watu wenye Ulemavu bila ya ya kuwabagua kwani kufanya hivyo ni kujiingiza katika dhambi zinazopaswa kulaaniwa.

No comments:

Post a Comment

Pages