Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi (kulia), akipokea zawadi
na vifaa kwa ajili ya Watu wenye Ulemavu Zanzibar kutoka kwa Balozi wa
Kuweit Nchini Tanzania Bwana Jasem Al – Najem.
Zanzibar
Zanzibar
Serikali ya Kuweit imeihakikishia Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kuendelea kuiunga mkono katika harakati zake za
kuimarisha ustawi wa Wananchi wake pamoja na miradi ya maendeleo.
Hatua hiyo itakwenda sambamba na Mpango Maalum
uliobuniwa na Ofisi ya Ubalozi wa Kuweit Nchini Tanzania katika kusaidia Vifaa
pamoja na zana za Kisasa zitakazowawezesha Watu wenye ulemavu kutengeneza vitu
vya sanaa katika kiwango cha Kitaalamu.
Balozi wa Kuweit Nchini Tanzania Bwana Jassem Al – Najem alitoa kauli hiyo wakati
akikabidhi zawadi ya Vifaa vya Viti,
Magongo, Miwani Pamoja na Mbao za
kusomea kwa ajili ya Wananchi wenye mahitaji maalum Zanzibar hapo Ofisi ya
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Vuga Mjini Zanzibar.
Zawadi hizo alizokabidhiwa Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi imegharimu Dola za Kimarekani Laki Tano sawa na
shilingi za Kitanzania Bilioni 1.1.
Balozi Jassem alisema jitihada zinazochukuliwa na
Kuweit katika kusaidia huduma za Kijamii katika Mataifa Rafiki yale yenye
mahitaji maalum alizieleza kuwa zitakuwa endelevu.
Balozi wa Kuweit Nchini Tanzania kupitia shughuli
hiyo maalum alitoa mkono wa pole kwa Wanzania na Watanzani wote kufuatia vifo
vya Askari 14 wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania { jwtz} waliouawa huko DRC.
Balozi Jassem alisema kitendo kilichofanywa na waasi
wa ADF hakikubaliki kabisa Kimataifa kwa vile kimekwenda kinyume na sheria na
taratibu zilizowekwa na Umoja wa Amani katika maeneo yanayopatiwa ulinzi wa
amani.
Akitoa shukrani kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar kufuatia zawadi hiyo ya
Serikali ya Kuweit Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
alisema Vifaa hivyo ni mkombozi mkubwa kwa Watu wenye Ulemavu hapa Zanzibar.
Balozi Seif
alisema Watu wenye ulemavu hawakujitakia kuwa na maumbile waliyokuwa nayo bali ni kudra tuu za Mwenyezi
Muungu ambazo wanapaswa kuendana nazo katika misingi na utaratibu wa
ustahamilivu.
Alisema Jamii inapaswa kutambua kuwa na wao ni
walemavu watarajiwa. Hivyo alisisitiza umuhimu wa Wananchi kuendelea kuwaenzi
na kuwatunza Watu wenye Ulemavu bila ya ya kuwabagua kwani kufanya hivyo ni
kujiingiza katika dhambi zinazopaswa kulaaniwa.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
15/12/2017.
No comments:
Post a Comment