*Ataka madiwani, watumishi wajali maslahi ya wananchi
*Aonya wasipojirekebisha, Serikali itavunja Baraza la Madiwani
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amewakemea watumishi wa umma na madiwani ambao wameunda makundi
ndani ya Manispaa ya Songea kwa kuweka mbele maslahi yao binafsi na akawataka
wajirekebishe mara moja.
Ametoa onyo
hilo jana (Jumamosi, Desemba 23, 2017) wakati akizungumza na watumishi wa
manispaa na madiwani kwenye kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa shule ya
sekondari ya wasichana ya Songea, mjini Songea mkoani Ruvuma.
“Watumishi
wa umma ni lazima muelewe kwamba katika Halmashaurti zenu mnafanya kazi na
waheshimiwa madiwani sababu mnatekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi, na
mnapotekeleza majukumu yenu mzingatie maslahi ya umma. Mnalo jukumu la kuhakikisha
Halmashauri yenu inaongozwa kitaalamu,” alisema.
“Nanyi
waheshimiwa madiwani, mtambue kuwa mnaongoza wataalamu wa fani tofauti. Lakini
hapa Songea, madiwani mmeigawa Halmashauri, mnaiendesha vibaya. Miradi haiendi
vizuri kwa sababu mmejiingiza kwenye kujali maslahi yenu binafsi,” alisema
Waziri Mkuu.
“Mmebishana
sana katika miradi ya maji, ujenzi wa kituo cha mabasi kwa sababu kila mmoja
anataka mtu wake aingie. Wakati mwingine pesa zinatumwa, nyie mnaanza kubishana
tu, sasa ni mwisho. Mkitaka kutuangusha Serikali, ama tutawafukuza uanachama
ama tutavunja Halmashauri. Tunao uwezo wa kulivunja Baraza la Madiwani,”
alionya.
Waziri Mkuu
alitumia fursa hiyo kumpongeza Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Bi. Tina Sekambo
kwa uamuzi wake wa kuruhusu mradi mmoja uendelee baada ya kuona kuna malumbano ya
kimaslahi miongoni mwa madiwani.
“Mkurugenzi
chapa kazi, na usimuogope mtu yoyote, iwe ni Diwani au Mstahiki Meya. Simamia
sheria kama ulivyofanya kwenye mradi ambao ulileta maneno, ukaamua Naibu Meya
asaini nyaraka, na mradi ukaendelea. Kisheria, Naibu Meya anaruhusiwa kusaini,”
alisema.
Waziri
Mkuu alisema kuwa Serikali inakusanya kodi ili wananchi wapate maendeleo na
kwamba Serikali ya Awamu ya Tano haina subira na mtu anayeharibu kazi.
Aliwaagiza Mkuu wa Mkoa na Katibu Tawala wa Mkoa wasimamie kazi na yeyote atakayeleta
uzembe, wamripoti kwake.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu
amemuonya Afisa Elimu wa Manispaa hiyo, Bi. Edith Kangomba na kumtaka aache
tabia ya kuchochea migomo kwa madiwani.
“Mkurugenzi
wa Manispaa mpe taarifa akirudi kwamba tutamfukuza kazi kwa sababu
anashirikiana na baadhi ya madiwani kuleta migomo kwenye utekelezaji wa miradi.
Mwambie leo ninamuomya, siku nyingine nitamfukuza hapa hapa kwenye kikao,” alielekeza
Waziri Mkuu kwa vile Afisa Elimu huyo hakuwepo kwenye kikao hicho kwa sababu
yuko likizo.
“Nasema
hivi kwa sababu hao washirika wake, wako hapa hapa na wamesikia ujumbe huu.
Serikali inahangaika, tunaleta fedha ajili ya elimu, lakini zikifika mnachaguana,
na Manispaa yenu iko nyuma kielimu,” alisema.
Aliwataka
wakuu wa idara wasimamie idara zao na kuziongoza kwa uadilifu na kuwaeleza kuwa
Serikali inatambua upungufu wa watumishi unaozikabili Halmashauri nyingi uliosababishwa
na zoezi la uhakiki wa vyeti. “Tunaajiri kidogo kidogo kwa awamu ili kuziba
pengo la vyeti feki. Tunajua sekta za afya na elimu ndizo zimeathirika zaidi. Lakini
nasisitiza tena, tunataka watumishi waadilifu, waaminifu na wawajibikaji.
Endeleeni kuchapa kazi,” alisisitiza.
Waziri Mkuu
alimaliza ziara yake ya siku moja mkoani Ruvuma jana hiyohiyo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, DESEMBA 24, 2017.
No comments:
Post a Comment