WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amewataka vijana wanaioishi kwenye mikoa ambayo zao la korosho
linastawi wachangamkie kilimo cha zao hilo kwa sababu lina fursa nyingi.
“Mahitaji ya
korosho ni makubwa duniani, korosho zinatumika mahotelini na kwenye mikutano mikubwa,
zinatumika kwenye ndege, kwa hiyo bei yake lazima iwe kubwa,” alisema.
Ametoa wito huo
jana (Jumapili, Desemba 31, 2017) wakati akizindua kampeni ya kitaifa ya
upandaji mikorosho bora na mipya milioni 10 msimu wa 2017/2018 mjini Ruangwa,
mkoani Lindi. Kaulimbiu ya kampeni hiyo ni:
“Korosho ni dhahabu ya kijani, tuitunze, itutunze”.
Waziri Mkuu
alisema anaamini kuwa kijana yoyote mwenye nguvu ya kufanya kazi hawezi
kushindwa kulima zao hilo kwa sababu halihitaji uangalizi mkubwa. “Kijana yeyote
anaweza kulima zao hili kwa sababu ekari moja ina miche 37 hadi 40. Kuna mtu
atashindwa kuangalia miche 37 hadi ikue?” aliuliza.
Waziri Mkuu
alisema kilimo cha korosho ni rahisi lakini pia kilimo cha korosho ni rafiki wa
mazingira, kwani miti ikikua inatunza mazingira na inasaidia kuleta mvua.
Alisema mbali ya mikoa inayolima korosho ya Lindi, Mtwara, Ruvuma Pwani na
Tanga, kuna mikoa mingine ambayo udongo wake umepimwa na kubainika kuwa zao
hilo linaweza kustawi bila shida.
Aliitaja mikoa
hiyo kuwa ni Dodoma, Kigoma, Njombe, Songwe na kuongeza kuwa mikoa ya Singida
na Manyara iko mbioni kukamilisha uchunguzi wake.
“Leo tumeanza
usambazaji wa miche ya bure hapa Ruangwa ambao najua utafuatiwa na wilaya
nyingine hapa nchini. Nimeelezwa kwamba mche wenye kutoa mazao mengi ni wa
kuanzia miaka mitatu hadi saba, kwa umri huu miche ya korosho inaweza kuchanganywa
na mazao mengine kama ambavyo mtashauriwa na maafisa kilimo ili wakati wa
palizi ya hayo mazao, shamba lako la korosho libakie kuwa safi,” alisema.
Waziri Mkuu ambaye pia ni
Mbunge wa Ruangwa, yuko kwenye mapumziko ya mwisho wa mwaka jimboni kwake.
Mapema, akitoa taarifa ya taarifa ya uzalishaji wa miche ya
mikorosho msimu wa 2017/18 mkoani Lindi, Katibu Tawala wa mkoa huo, Bw. Ramadhani
Kaswa alimweleza Waziri Mkuu kwamba katika msimu wa 2016/2017, mkoa huo uliweka lengo la
kuzalisha na kupanda miche 1,000,000 ya mikorosho.
“Hadi mwisho wa msimu huu, jumla
miche 716,532 ilizalishwa na kusambazwa kwa wakulima sawa na asilimia 71.6 ya
lengo lililowekwa. Kati ya hiyo, Halmashauri ya Kilwa ilizalisha miche 55,000, Halmashauri
ya Lindi miche 100,000, Manispaa ya Lindi miche 50,000; Halmashauri ya Liwale
miche 106,000; Halmashauri ya Nachingwea miche 227,670 na halmashauri ya
Ruangwa miche 177,862,” alisema.
“Miche hii iligawanywa kwa
wakulima bure ambao walipanda kwenye mashamba yao. Zoezi la tathmini ya miche
iliyokua baada ya kupandwa linaendelea kwenye halmashauri zote za mkoa,”
aliongeza.
Bw. Kaswa alisema kutofikiwa
kwa lengo hilo kumechangiwa na kutopatikana kwa mahitaji yote ya mbegu na vifaa
vya uzalishaji, kuchelewa kwa vifaa, na mwamko mdogo wa vikundi vya uzalishaji.
Alisema kwa msimu huu wa
2017/2018, mkoa uliweka lengo la kuzalisha miche ya mikorosho iliyobebeshwa na
isiyobebeshwa 7,132,000. Kati ya hiyo, Wilaya ya Kilwa walilenga miche 1,122,000,
Lindi Vijijini 1,550,000, manispaa ya Lindi 1,000,000, Liwale miche 450,000,
Nachingwea miche 1,810,000 na Ruangwa miche 1,200,000.
“Hadi kufikia tarehe 29
Desemba, 2017 tayari miche 4,974,425 ilikuwa imezalishwa na iko tayari kwa kupandwa
kwenye mamlaka za serikali za mitaa kama ifuatavyo:- Kilwa miche 772,000, Lindi
Vijijini 1,160,455, manispaa ya Lindi 771,440, Liwale miche 266,000, Nachingwea
991,070 na halmashuri ya Ruangwa imezalisha miche 1,013,460,” alisema.
Sherehe hizo za
uzinduzi wa upandaji miche mipya zilihudhuriwa na wakuu wa mikoa ya Lindi,
Mtwara, Ruvuma, Pwani na wajumbe wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT). Wakuu wa
Wilaya, baadhi ya Wenyeviti wa Halmashauri na wataalamu kutoka kituo cha
utafiti cha Naliendele walishiriki uzinduzi huo.
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU,
JANUARI MOSI, 2018.
No comments:
Post a Comment