Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amesema
maboresho ya TEHAMA yanayofanywa na mhimili wa mahakama nchini utasaidia
kupunguza foleni za wananchi wanaofika ofisi za Wakuu wa Wilaya na kwa Mkuu wa
Mkoa kutafuta haki zao.
Amesema kuwa kitendo cha mwaanchi kuweza kujua mwenendo
wa kesi bila ya kufika mahakamani ni maendeleo makubwa yanayofikiwa na mhimili
huo na kuwaasa kuanza kufanya kazi baada ya kuwa likizo ya mwisho wa mwaka.
Ameyasema hayo kwenye maadhimisho ya wiki ya sheria
ambayo hufanyika tarehe 1, Februari ya kila mwaka katika Viwanja wa mahakama
kuu ya Tanzania kanda ya Sumbawanga inayojumuisha mikoa ya Rukwa na Katavi.
“Mwaka 2018 na jitihada zilizofanyika na mahakama umekuwa
mwanzo mzuri, wananchi watajitokeza kutafuta elimu hii ya sheria na wanapoipata
itatupunguzia msongamano kwenye ofisi zetu za Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa
ili tufanye kazi za maendeleo sio kusuluhisha migogo ya ndoa, mirathi na ardhi
ambayo yote imekaa katika misingi ya kisheria,” Alieleza.
Na kuongeza kuwa elimu hii ya sheria iendelee kutolewa
ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wakati huku wakizingatia kaulimbiu ya
maadhimisho hayo inayosema “Matumizi ya TEHAMA kwa kutoa haki kwa wakati na
kuzingatia maadili.”
Kwa upande wake Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu ya Tanzania
kanda ya Sumbawanga John Mgeta ametahadahrisha matumizi mabaya ya Teknolojia
katika kuvunja maadili na misingi ya mahakama na utu kwani watu hutumia
teknolojia hiyo kuendeleza rushwa kupitia namba za simu za mahakama.
“Mtumishi wa mahakama anaweza kutumia simu kuwasiliana na
mtu akimuomba rushwa au kufanya miamala ya pesa, vyombo vya habari na wananchi
ambao wanakiuka maadili kwa kutumia simu na TEHAMA, sisi tunasisitiza matumizi
haya yazingatie maadili,” Alibainisha.
Awali akitoa taarifa ya chama cha wanasheria Tanzania Wakili
Baltazar Chambi amesema kuwa mahakama ya Tanzania kwa kutumia TEHAMA itafikia
suluhu mojawapo ya uhakika wa utoaji wa haki kwa wakati kwa kulitambua hilo
wadau wa haki ni vyema wakajua matumizi ya TEHAMA ili kuleta ufanisi katika
kazi zao.
No comments:
Post a Comment