*Ni baada ya kuisababishia halmashauri hasara
ya sh. milioni
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa
amemsimamisha kazi Mwanasheria wa Halmashauri
ya wilaya ya Misungwi Bw. Alphonce Sebukoto na kuagiza achungunzwe na vyombo
husika.
Amechukua hatua hiyo baada Mwanasheria huyo kushindwa
kutekeleza majukumu yake ipasavyo ikiwa ni pamoja na kushindwa kuishauri vema
halmashauri hiyo na kuisababishia hasara ya sh. milioni 279.
Waziri Mkuu amemsimamisha
kazi Bw. Sebukoto leo (Jumatatu,
Februari 19, 2018) wakati akizungumza na watumishi na madiwani wa halmashauri
hiyo akiwa katika siku ya tano ya ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza.
“Mwanasheria
utasimama kazi kuanzia leo na tuhuma zako zitachunguzwa kikamilifu na vyombo
husika na uchunguzi ukibaini kama huna kosa utarudi kazini. Hatuta kuonea
lakini hatuwezi kukuvumilia kwa utaratibu huo ulioufanya.”
Amesema mwanasheria huyo Novemba 2017 wakati alipokuwa
anakaimu nafasi ya ukurugenzi aliidhinisha malipo ya sh.milioni 279 zilipwe
katika akaunti binafsi ya Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Bw. Anthony Bahebe.
Waziri Mkuu amesema Bw. Bahebe aliishtaki halmashauri hiyo
akidai kulipwa fedha kwa ajili ya kazi ya ukandarasi wa mradi wa maji Igenge uliojengwa
na kampuni ya ukandarasi ya Seekevim.
Amesema mradi huo ulianza 2014 na ulitakiwa ukamilike 2015.
Mwanasheria huyo aliidhinisha malipo hayo wakati ambao tayari hati maalumu ya
uwakilishi ilikuwa imekwisha tangu Desemba 2015.
“Mwanasheria amemlipa Mwenyekiti wa Halmashauri kwa kufanya
kazi na Halmashauri baada ya kuifikisha Halmashauri yake Mahakamani. Amemlipa
fedha wakati kazi yenyewe ilikuwa haijaisha na aliharakisha malipo hayo kipindi
ambacho Mkurugenzi hayupo.”
Waziri Mkuu amewakumbusha watumishi wa umma kuzingatia
maadili ya utumishi na matakwa ya kisheria katika utekelezaji wa majukumu yao.
Amesema fedha alizolipwa Bw. Bahebe zingeweza kutumika katika ujenzi wa miradi
mbalimbali ya maendeleo katika halmashauri hiyo.
Awali, Waziri Mkuu alifungua mabweni ya
watoto wenye mahitaji maalumu katika shule ya msingi Mitindo iliyoko wilayani
Misungwi na kisha alikagua ujenzi wa vyumba vya madarasa.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, FEBRUARI 19,
2018.
No comments:
Post a Comment