*Ni baada ya kuisababishia halmashauri hasara ya sh. milioni
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwaamemsimamisha kazi Mwanasheria wa Halmashauri ya wilaya ya Misungwi Bw. Alphonce Sebukoto na kuagiza achungunzwe na vyombo husika.
Amechukua
hatua hiyo baada Mwanasheria huyo kushindwa kutekeleza majukumu yake
ipasavyo ikiwa ni pamoja na kushindwa kuishauri vema halmashauri hiyo na
kuisababishia hasara ya sh. milioni 279.
Waziri Mkuu amemsimamisha kazi Bw. Sebukoto leo (Jumatatu,
Februari 19, 2018) wakati akizungumza na watumishi na madiwani wa
halmashauri hiyo akiwa katika siku ya tano ya ziara yake ya kikazi
mkoani Mwanza.
“Mwanasheria
utasimama kazi kuanzia leo na tuhuma zako zitachunguzwa kikamilifu na
vyombo husika na uchunguzi ukibaini kama huna kosa utarudi kazini.
Hatuta kuonea lakini hatuwezi kukuvumilia kwa utaratibu huo ulioufanya.”
Amesema
mwanasheria huyo Novemba 2017 wakati alipokuwa anakaimu nafasi ya
ukurugenzi aliidhinisha malipo ya sh.milioni 279 zilipwe katika akaunti
binafsi ya Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Bw. Anthony Bahebe.
Waziri
Mkuu amesema Bw. Bahebe aliishtaki halmashauri hiyo akidai kulipwa
fedha kwa ajili ya kazi ya ukandarasi wa mradi wa maji Igenge uliojengwa
na kampuni ya ukandarasi ya Seekevim.
Amesema
mradi huo ulianza 2014 na ulitakiwa ukamilike 2015. Mwanasheria huyo
aliidhinisha malipo hayo wakati ambao tayari hati maalumu ya uwakilishi
ilikuwa imekwisha tangu Desemba 2015.
“Mwanasheria
amemlipa Mwenyekiti wa Halmashauri kwa kufanya kazi na Halmashauri
baada ya kuifikisha Halmashauri yake Mahakamani. Amemlipa fedha wakati
kazi yenyewe ilikuwa haijaisha na aliharakisha malipo hayo kipindi
ambacho Mkurugenzi hayupo.”
Waziri
Mkuu amewakumbusha watumishi wa umma kuzingatia maadili ya utumishi na
matakwa ya kisheria katika utekelezaji wa majukumu yao. Amesema fedha
alizolipwa Bw. Bahebe zingeweza kutumika katika ujenzi wa miradi
mbalimbali ya maendeleo katika halmashauri hiyo.
Awali,
Waziri Mkuu alifungua mabweni ya watoto wenye mahitaji maalumu katika
shule ya msingi Mitindo iliyoko wilayani Misungwi na kisha alikagua
ujenzi wa vyumba vya madarasa.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, FEBRUARI 19, 2018.
No comments:
Post a Comment