WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imefanikiwa kurejesha
mali tisa kati ya 10 za Chama Kikuu cha Ushirika cha Nyanza (NCU) ambazo
zilichukuliwa kinyume cha taratibu na kuagiza watuhumiwa wachukuliwe hatua za
kisheria.
Amesema mali moja iliyobakia bado inafanyiwa uchunguzi na mali mbili za
Chama Kikuu cha Ushirika cha Shinyanga (SHIRECU) nazo pia zimepatikana lakini
bado ziko kwenye hatua ya makabidhiano.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Februari 9, 2018) bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa 10 wa
Bunge la 11. Bunge limeahirishwa hadi Aprili 3, mwaka huu.
Waziri Mkuu amezitaja mali za Chama Kikuu cha Ushirika cha Nyanza (NCU) zilizorejeshwa
kuwa jengo la Nyanza Cooperative Union (1984) Ltd. maarufu
kwa jina la “Transport House” au KAUMA House, lililopo katika kiwanja namba
242, Kitalu T, Mtaa wa Stesheni; kiwanda cha kusindika mafuta cha New Era Oil
Mill, kilichopo katika eneo la Igogo; na jengo na viwanja vya Ashock Industries
vilivyopo eneo la viwanda Igogo.
Nyingine
ni majengo ya kilichokuwa kiwanda cha mkonge na dengu kilichopo eneo la Igogo kwenye kiwanja
namba 41 na 79; jengo lililopo
katika kiwanja kilichopo Isamilo namba
80, kitalu “D”; jengo lililopo katika kiwanja kilichopo Isamilo namba 110, kitalu
“D” na ghala moja katika kiwanja namba 104, kitalu “A” kilichopo eneo la Igogo.
“Mali
nyingine zilizorejeshwa ni jengo moja lililopo mjini Geita katika kiwanja namba
8 Kitalu “K”; jengo moja lililopo mjini Geita, katika kiwanja namba 24, Kitalu
“K” na jengo lililopo Isamilo katika kiwanja namba 89 Kitalu “D”,” amesema
Waziri Mkuu.
Kwa
upande wa mali za SHIRECU, Waziri Mkuu amezitaja mali zilizopo kwenye hatua ya
makabidhiano kuwa ni ghala lililopo Kurasini, Dar es Salaam na nyumba ya
ghorofa tatu iliyopo kiwanja namba 1001 “BB” Ilala, jijini Dar es Salaam.
“Katika kusimamia misingi ya utawala bora na uwajibikaji wa watendaji wa
vyama vya ushirika, Serikali inaendelea kufanya uchunguzi maalum kuhusu
mikataba mibovu ya Chama Kikuu cha Ushirika cha Nyanza (NCU), Chama Kikuu cha
Ushirika cha Shinyanga (SHIRECU), Chama Kikuu cha Ushirika cha Kagera (KCU) na
Chama Kikuu cha Ushirika cha Kilimanjaro (KNCU). Vilevile, tunachunguza kushikiliwa
kwa mali za ushirika bila kufuata utaratibu,” amesema.
Amesema Serikali itaendelea kuviamsha vyama vya ushirika vya msingi na
vyama vikuu vilivyosinzia katika mikoa yote ili kujenga ushirika imara na
kwamba juhudi na hatua hizo zinazochukuliwa na Serikali, zinalenga kuongeza
imani, hamasa na uzalishaji wa mazao na kusimamia masoko yake, na hivyo, kuinua
kipato cha wakulima sambamba na kuwapatia fursa ya kujiajiri wenyewe katika
sekta ya kilimo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S.
L. P. 980,
41193 - DODOMA.
IJUMAA, FEBRUARI 9, 2018.

No comments:
Post a Comment