WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema hali ya usalama wa chakula
nchini imeimarika kutokana na uzalishaji mzuri wa mazao ya chakula.
Aliyasema hayo jana
(Ijumaa, Februari 9, 2018) bungeni mjini Dodoma wakati
akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa 10 wa Bunge la 11. Bunge limeahirishwa
hadi Aprili 3, mwaka huu.
Waziri Mkuu alitaja mazao hayo kuwa ni pamoja na mahindi yaliyovunwa katika mikoa
ya Ruvuma, Njombe, Iringa, Katavi, Kigoma, Mbeya, Songwe na Rukwa.
“Matarajio yetu kuwa hali ya mavuno msimu huu itakuwa nzuri kwa sababu mwenendo
wa unyeshaji wa mvua za vuli ulikuwa wa kuridhisha katika maeneo mengi nchini.”
Alisema Serikali inaendelea
kusimamia na kuhakikisha kuwa hali ya utengamano na usalama wa chakula unaendelea
kuwa imara kwa wananchi wote na kwa wakati wote.
Waziri Mkuu alisema
Serikali inawezesha wafanyabiashara wa mazao ya chakula kuendelea kusafirisha
na kuuza mazao ya chakula nje na ndani ya nchi.
Hivyo, Waziri Mkuu
alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wakulima waendelee kuzitumia vizuri mvua
zinazoendelea kunyesha kwa kupanda mazao stahiki na kutumia chakula
walichonacho kwa uangalifu hadi msimu mwingine wa mavuno.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu
alisema upatikanaji na usambazaji wa pembejeo kwa
wakulima umeimarika, ambapo takwimu zinaonesha kwamba hadi kufikia Februari
Mosi, 2018 upatikanaji wa mbolea nchini kwa ajili ya mahindi na tumbaku
ulifikia tani 250,376 sawa na
asilimia 51.6 ya wastani wa
mahitaji ya tani 485,000 kwa
mwaka.
“Katika kipindi
hicho hicho, mbolea za kupandia na kukuzia zipatazo tani 229,839 ziliingizwa nchini na
kusambazwa mikoani. Upatikanaji wa dawa za maji na unga (Salfa) kwa ajili ya
mazao ya pamba na korosho unaendelea.”
Waziri Mkuu alisema hadi
kufikia Februari Mosi, 2018 upatikanaji wa mbegu bora nchini ulifikia
tani 51,700, sawa na asilimia 86.2 ya mahitaji halisi ya tani 60,000 kwa
mwaka. Katika kipindi hicho
jumla ya tani 22,357 za mbegu
bora zilisambazwa nchini.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 - DODOMA.
JUMAMOSI, FEBRUARI 10,
2018.
No comments:
Post a Comment