WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amemuagiza kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Mtwara Bw. Stephen Mafipa kumtafuta
popote alipo na kumkamata aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Masasi
Bw. Fortunatus Kagoro kwa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha.
Mbali na Bw. Kagoro pia Kaimu Mweka Hazina Bw.
Heri Hamad Afisa Mipango Bi Teresia Nsumba nao ameagiza wakamatwe na
baada ya uchunguzi watakaobainika kwamba hawajahusika na ubadhilifu huo
watarudishwa kazini. "Lazima fedha za Serikali zitumike kama ilivyokusudiwa."
Watendaji hao wanadaiwa kutumia sh. bilioni
1.8 zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Halmashauri ya Mji
wa Masasi kwa kuchora mchoro na kujenga msingi katika maeneo mawili tofauti.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatatu,
Februari 26, 2018) wakati akizungumza na watumishi na Madiwani wa Halmashauri
ya Mji wa Masasi na Halmashauri ya wilaya ya Masasi akiwa kwenye ziara yake ya
kikazi mkoani Mtwara.
Amesema mwaka 2014 Serikali ilipeleka sh
milioni 575 wilaya Masasi kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Halmashauri hiyo na
fedha hizo ziliishia kutumika katika hatua za maandalizi ya awali ikiwa
ni pamoja na kutengeneza michoro ya jengo.
Waziri Mkuu amesema 2016/2017 Serikali
ilipeleka tena sh. bilioni 1.25 kwa ajili ya ujenzi huo, ambapo Halmashauri
hiyo ilienda kutafuta eneo lingine na kufanya tena shughuli zilizokuwa
zimefanyika na kuanza ujenzi ambao umeishia katika msingi na fedha zimeisha.
Pia amewataka watendaji hao kutotumia fedha za
makusanyo ya ndani kwa ajili ya kuziba pengo la fedha za mradi huo ambazo
baadhi yake hazijulikani zilipo na amewaagiza Madiwani kutoruhusu jambo
hilo.
"Madiwani msikubali kutumia fedha za
makusanyo ya ndani kupeleka kwenye ujenzi wa miradi ya maendeleo ambayo tayari
Serikali ilishatoa fedha ya ujenzi wake.
Amesema Serikali inahitaji kuona fedha za
maendeleo zinazopelekwa katika Halmashauri mbalimbali nchini zinatumika kama
ilivyoelekeza na si vinginevyo na Serikai haitakuwa na mzaha kwa mtumishi
atakayezitumia vibaya.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, FEBRUARI 26,
2018.
No comments:
Post a Comment