WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa viwanda
vikubwa viwili vya kuchakata pamba ambao wameahidi kununua pamba yote
itakayozalishwa nchini kuanzia msimu huu.
Viongozi
hao ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Namera Group of Industries Bw. Hamza
Rafiq Pardesi na Mkurugenzi Mtendaji wa JOC Bw. Qin Mengwei ambao kwa pamoja
wameahidi kununua pamba yote itakayozalishwa.
Waziri Mkuu amekutana na viongozi hao leo
(Jumatatu, Februari 12, 2018) jijini
Dar es Salaam na amesema kwamba wakulima
waliitikia wito wa Serikali wa kufufua zao hilo, hivyo mwaka huu wanatarajia
kupata mavuno mengi.
Waziri
Mkuu amewataka viongozi hao wajiandae kununua pamba nyingi kwa sababau mwaka huu
wakulima wamelima pamba ya kutosha baada ya Serikali kuwahamasiha waongeze
uzalishaji kwa kuwa kuna soko la uhakika.
Amesema hatua hiyo imekuja baada ya
Rais Dkt. John Magufuli kutoa maelekezo ya uhamasishaji wa kilimo hasa mazao
makuu ya biashara, tayari tija
imeanza kuonekana ambapo zao la korosho limepata mafanikio makubwa na sasa
linafuatia zao la pamba.
Waziri Mkuu amesema Serikali inashiriki kikamilifu katika usimamizi wa
zao la pamba kuanzia hatua za maandalizi ya shamba kwa wakulima kuelekezwa
kulima kitaalam, upatikanaji wa pembejeo hadi masoko, hivyo amewaalika viongozi
hao kushiriki katika mkutano utakaowakutanisha wafanyabiashara wote wa zao
hilo.
“Mimi mwenyewe mwezi huu nitakuwa na ziara ya kikazi mkoani Mwanza, kwa
hiyo tarehe 21, Februari, nimeitisha mkutano wa wafanyabiashara wote wa pamba
nchini iwe ni wanaosokota nyuzi, kuchambua pamba au kukamua mbegu za pamba, ili
mradi wanajihusisha na pamba nanyi naomba muwepo”.
Waziri Mkuu amesema Serikali imefurahishwa na uamuzi wao wa kutaka kununua
pamba yote itakayozalishwa nchini kuanzia msimu huu kwani ni faraja kwa Taifa
kwa sababu wakulima walipunguza uzalishaji baada ya kukosa soko la uhakika.
Kwa upande
wao, Bw. Pardesi na
Bw. Qin wamemuhakikishia Waziri Mkuu kwamba kampuni zao zinauwezo wa kununua
pamba yote inayozalishwa nchini na kuichakata katika viwanda vyao na
kutengeneza nyuzi na nguo zitakazouzwa nchini kwa bei nafuu.
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU,
FEBRUARI 12, 2018.
No comments:
Post a Comment