WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Mpango Mkakati wa Afya Moja na Dawati
la Kuratibu Afya Moja nchini ni muhimu katika kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa mahala
safi na salama kwa kuishi na kufanya kazi za kimaendeleo.
Ametoa
kauli hiyo leo (Jumanne, Februari 13, 2018) wakati akizindua mpango mkakati huo
katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam, ambapo amesema dhana ya Afya Moja inafaa kutumika zaidi katika nchi
zinazoendelea.
Waziri
Mkuu amesema mbali na mpango kufaa kutumika katika nchi zinazoendelea pia hata
kwa nchi zinazokaribia maeneo ya wanyama pori kama Tanzania kutokana na
kukabiliwa na changamoto ya upungufu wa rasilimali.
Amesema
kwa upande wa nchi za Afrika hali ni hatarishi zaidi kwa kuwa Bara hilo, lina
sehemu nyingi zinazokaribia mapori makubwa ya wanyama kama Bonde la Mto Kongo,
ambalo mazingira yake yamekuwa ni kitovu cha magonjwa ya mlipuko kama vile
Ebola, Homa ya Bonde la Ufa (RVF), Marburg na mengineyo.
Waziri Mkuu amesema kwa kutambua hilo, Serikali kwa
kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID) na wadau wengine wa
Maendeleo, imeendelea kutekeleza agenda ya Afya Moja nchini tangu mwaka 2013
ilipozinduliwa kwa mara ya kwanza mjini Arusha na Makamu wa Rais Mstaafu, Dkt. Mohamed Gharib
Bilal.
“Utekelezaji wa Mpango huu unakwenda sambamba na maelekezo
ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (2015-2020) ya kujenga Taifa lenye
watu wenye afya bora itakayowawezesha kuzalisha mali na kutoa huduma mbalimbali
ambayo ni muhimu sana katika kufikia azma ya Serikali ya kujenga Uchumi wa
Viwanda.”
Awali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
Sera, Bunge,Kazi,Vijana,Ajira na Wenye Ulemavu, Bibi Jenista Mhagama alisema
uzinduzi wa mkakati huo ni ngao tosha kwa nchi katika kuzuia na
kudhibiti magonjwa.
Alisema
pamoja na kutekeleza kanuni za Kitaifa, Kikanda na Kimataifa ambazo zinahitaji
ushirikiano wa sekta mbalilmbali kwa
kutumia dhana ya afya moja, mpango mkakati huo unaleta msukumo katika Ofisi ya
Waziri Mkuu kuendelea kushirikiana na
Taasisi mbalimbali kudhibiti magonjwa.
Bibi Jenista
alisema uratibu wa afya
moja unakwenda sambamba na matakwa ya Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika
linaloshughulika na Afya ya Wanyama (IOE) na Shirika la Kimataifa la Chakula la
Kilimo (FAO) ambayo yanashirikiana katika kudhibiti magonjwa yanayoambukiza na
usugu wa dawa.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, FEBRUARI 13,
2018.
No comments:
Post a Comment