Kikao cha
Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF ilikutana
Jumamosi Februari 10, 2018 kupitia mashauri yaliyofikishwa kwenye kamati hiyo.
Shauri namba moja lilihusisha malalamiko dhidi ya
wachezaji Saba(7) wa timu ya Transit Camp,shauri ambalo lilihudhuriwa na
mchezaji mmoja Mohamed Suleiman Ussi.
Mchezaji Mohamed Suleiman Ussi alituhumiwa kwa kosa la
utovu wa nidhamu kwenye mechi namba 48 ya Kundi C Ligi Daraja la Kwanza
Tanzania Bara akidaiwa kutaka kumpiga Mwamuzi wa mchezo kinyume na Ibara ya
50(1)(2) na (5)ya Katiba ya TFF toleo la 2015.
Kamati ilipitia ripoti ya kamishna wa mechi ambayo pamoja
na kuwataja wachezaji wengine wengine pia ilimtaja Mohamned Suleiman Ussi
kuhusika kwenye tukio hilo akiwa amevaa jezi namba 14 ambaye pia alitajwa
kwenye ripoti ya mwamuzi ikielezea kitendo cha Mohamed Suleiman Ussi kutaka
kumpiga mwamuzi msaidizi namba 2.
Baada ya kupitia ripoti Kamati imejiridhisha kuwa mchezaji
Mohamed Suleiman Ussi alitaka kumpiga mwamuzi kinyume na kanuni ya 36 ya Ligi
Daraja la Kwanza na ibara ya 50(1)(2) na
(5) ya Katiba ya TFF toleo la 2015.
Kamati imemuadhibu Mohamed Suleiman Ussi imemfungia
kutocheza michezo mitatu(3) pamoja na faini ya Shilingi laki tatu(300,000) kwa
mujibu wa kanuni ya 37(7) na 37(12) kanuni za Ligi Daraja la Kwanza.
KAMATI
YA NIDHAMU YAMFUNGIA JUMA NYOSO
Kamati ya Nidhamu iliyokutana Jumamosi Februari 10, 2018
pamoja na mambo mengine pia ilipitia shauri la mchezaji wa Kagera Sugar Juma
Nyoso lililofikishwa kwenye kamati akituhumiwa kwa utovu wa nidhamu kwenye
mechi namba 112 ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Kagera Sugar dhidi ya
Simba Sports Club iliyochezwa kwenye Uwanja wa Kaitaba.
Juma Nyoso alituhumiwa kumpiga shabiki baada ya kumalizika
mchezo huo kinyume cha kanuni ya 36 ya ligi Kuu inayozungumzia uchezaji wa
kiungwana pamoja na Ibara 50(1)(2) na (5) ya katiba ya TFF toleo la 2015.
Kamati ilipitia ripoti ya kamishna wa mechi ambayo
imeeleza tukio hilo la Juma Nyoso kupishana na shabiki aliyekuwa amebeba
vuvuzela na ndipo Nyoso aliposimama na
kuanza kumpiga na kiatu na kutumia goti mpaka askari wa jeshi la Polisi
walipoingilia kumuokoa na kumshikilia mchezaji huyo wakati shabiki akipatiwa
huduma kwenye gari la huduma ya kwanza.
Juma Nyoso katika utetezi wake alikana malalamiko dhidi
yake akidai kitendo alichofanya ni kukunjana na shabiki.
Kamati kupitia ripoti ya kamishna wa mchezo huo imemtia
hatiani Juma Nyoso kupitia kanuni ya 36 ya kanuni ya Ligi kuu na Ibara ya
50(1)(2) na (5) ya katiba ya TFF.
Kamati pia ilipokea taarifa za nyuma za nidhamu za Juma
Nyoso ambayo rekodi inaonesha aliwahi kufungiwa kwa makosa ya kinidhamu .
Kupitia kifungu cha 37(10)cha kanuni za ligi Kuu kamati
imemtia hatiani Juma Nyoso na imemfungia kutocheza mechi Tano(5) na faini ya
Shilingi milioni moja(1,000,000).
MAAMUZI
KAMATI YA SAA 72
LIGI KUU
YA VODACOM
Mechi
namba 122 (Lipuli 0 vs Yanga 2). Klabu za Lipuli na Yanga
kila moja imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kutumia milango isiyo
rasmi kuingia uwanjani, kitendo ambacho ni ukiukaji wa Kanuni ya 14(14) ya Ligi
Kuu. Adhabu dhidi yao imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu
kuhusu Taratibu za Mchezo.
Pia klabu
ya Yanga imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kutoingia vyumbani,
hivyo kwenda kinyume na Kanuni ya 14(13) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Adhabu hiyo ni uzingativu wa Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za
Mchezo.
Mechi
namba 123 (Singida United 3 vs Mwadui 2). Kocha wa makipa wa Mwadui,
Lucheke Gaga amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano)
baada ya kuondolewa kwenye benchi (ordered off) na Mwamuzi kwa kutoa lugha ya
matusi katika mechi hiyo iliyofanyika Februari 3, 2018 kwenye Uwanja wa Namfua
mjini Singida. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 40(11) ya Ligi
Kuu kuhusu Udhibiti wa Makocha.
Mechi
namba 128 (Ruvu Shooting 0 vs Simba 4). Mchezaji wa Ruvu Shooting,
Mau Bofu amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa
kumpiga kiwiko Emmanuel Okwi wa Simba katika mechi hiyo iliyofanyika Februari
4, 2018 kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam. Adhabu hiyo imezingatia
Kanuni ya 37(3) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Wachezaji.
LIGI DARAJA LA KWANZA
Mechi namba 53 Kundi A (Kiluvya United 0 vs African Lyon 1). Klabu ya
African Lyon imepigwa faini ya sh. 200,000 (laki mbili) kutokana na timu yake
kutoingia vyumbani katika mechi hiyo iliyofanyika Februari 5, 2018 kwenye
Uwanja wa Filbert Bayi mkoani Pwani.
Kitendo hicho ni ukiukaji wa Kanuni ya 14(13) ya Ligi Daraja la
Kwanza kuhusu Taratibu za Mchezo. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni
ya 14(49) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mechi namba 53 Kundi B (Mawenzi Market 0 v Coastal Union 2). Klabu ya
Mawenzi Market imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na washabiki
wake kuwarushia chupa Waheshimiwa Mawaziri ambao ni washabiki wa Coastal Union
katika mechi hiyo iliyofanyika Februari 2, 2018 kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini
Morogoro.
Adhabu dhidi ya klabu ya Mawenzi Market imetolewa kwa kuzingatia
Kanuni ya 42(1) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Klabu.
Mechi namba 53 Kundi C (Alliance Schools 2 vs JKT Oljoro 1). Wachezaji
Ramadhani Yego na Joseph Mkota wa JKT Oljoro wanapelekwa Kamati ya Nidhamu ya
TFF kwa kutaka kumpiga Mwamuzi baada ya kumalizika mechi hiyo iliyochezwa
Februari 4, 2018 kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.
LIGI DARAJA LA PILI
Mechi namba 28 Kundi B (Kilimanjaro Heroes 0 v Pepsi 2). Klabu ya
Kilimanjaro Heroes imepigwa faini ya sh. 200,000 (laki mbili) kwa kuhudhuria
kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting) katika mechi hiyo
iliyofanyika Februari 3, 2018 katika Uwanja wa Ushirika mjini Moshi, kinyume na
Kanuni ya 14(2b) ya Ligi Daraja la Pili kuhusu Taratibu za Mchezo.
Adhabu dhidi ya Kilimanjaro Heroes imetolewa kwa kuzingatia Kanuni
ya 14(3) ya Ligi Daraja la Pili kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mechi namba 30 Kundi B (African Sports 2 v AFC 0). Wachezaji
wa AFC, John George Rasta na Shaibu Salim wanapelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF
kwa kutaka kumshambulia Mwamuzi kabla ya kuokolewa na viongozi wa timu hiyo
katika mechi hiyo iliyofanyika Februari 3, 2018 katika Uwanja wa Mkwakwani
jijini Tanga.
Klabu ya AFC imepigwa faini ya sh. 200,000 (laki mbili) kwa
kutoingia vyumbani wakati wa mapumziko, kitendo ambacho ni kinyume na Kanuni ya
14(13) ya Ligi Daraja la Pili kuhusu Taratibu za Mchezo. Adhabu hiyo imetolewa
kwa kuzingatia Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
MALALAMIKO YA NJOMBE MJI
Klabu ya Njombe Mji
iliwasilisha malalamiko kuwa Tanzania Prisons ilimchezesha mchezaji James
Mwasote katika mechi yao namba 126 ya Ligi Kuu ya Vodacom iliyofanyika Februari
3, 2018 wakati akiwa na kadi tatu za njano.
Kamati imekataa malalamiko
ya Njombe Mji FC kwa vile wakati James Mwasote anacheza mechi hiyo iliyofanyika
Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya alikuwa na kadi mbili za njano.
Mwasote alipata kadi hizo kwenye mechi dhidi ya Majimaji na dhidi ya Singida
United.
IMETOLEWA
NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA TFF
No comments:
Post a Comment