Viongozi wa Chadema wakiwa ndani ya gari la Polisi wakati walipofika katika Mahakama ya hakimu mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam wakikabiliwa na mashtaka ya kuchochea uasi.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akisalimiana na Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Prof. Abdallah safari katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.
Viongozi
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wakiwa katika chumba
cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam wakikabiliwa na mashtaka manane yakiwemo ya kuchochea uasi. Kutoka
kushoto ni Naibu Katibu Mkuu (Bara), John Mnyika; Mwenyekiti wa Chadema
Taifa, Freeman Mbowe; Katibu Mkuu, Dk. Vincent Mashinji; Mbunge wa
Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa na Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar),
Salum Mwalimu.
Mwenyekiti
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, pamoja
na viongozi wenzake wa chama hicho wakiwa ndani ya gari la Polisi
wakipelekwa mahabusu ya Gereza la Segerea jijini Dar es Salaam
baada ya kusomewa mashtaka manane yakiwemo ya kuchochea uasi. (Picha
na Francis Dande).
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, pamoja na viongozi wenzake wa chama hicho wakiwa ndani ya gari la Polisi wakipelekwa mahabusu ya Gereza la Segerea jijini Dar es Salaam baada ya kusomewa mashtaka manane yakiwemo ya uchochezi wa uasi. (Picha na Francis Dande).
HATIMAYE utabiri wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, kuwa viongozi na wabunge wa chama hicho watafunguliwa kesi na kutupwa gerezani umetimia.
Machi 22, mwaka huu, Mbowe aliibua madai mazito kuwa baadhi ya watendaji wa serikali wana mkakati wa kuwabambikizia kesi ya uhaini, ugaidi au mauaji viongozi wakuu wa chama hicho ambao wamekuwa wakiripoti Polisi kwa muda mrefu bila kuambiwa kosa lao.
Machi 22, mwaka huu, Mbowe aliibua madai mazito kuwa baadhi ya watendaji wa serikali wana mkakati wa kuwabambikizia kesi ya uhaini, ugaidi au mauaji viongozi wakuu wa chama hicho ambao wamekuwa wakiripoti Polisi kwa muda mrefu bila kuambiwa kosa lao.
Jana viongozi sita wa Chadema walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka manane yakiwemo ya uchochezi wa uasi.
Walioshtakiwa ni Mbowe; Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa; Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar). Salum Mwalimu; Naibu Katibu Mkuu (Bara) na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika; Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Vincent Mashinji.
Hata hivyo baada ya kusomewa mashtaka hayo Mbowe na wenzake walipelekwa rumande hadi kesho kwa ajili ya uamuzi wa dhamana.
Akisoma mashtaka hayo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Faraja Nchimbi, akisaidiana na Dk. Zainabu Mango, alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, kuwa washtakiwa kwa pamoja walitenda makosa hayo Februari 16, mwaka huu maeneo ya viwanja vya Buibui na Barabara ya Kawawa, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam.
Katika shtaka la kwanza wanatuhumiwa kufanya mkusanyiko usio halali kinyume cha sheria.
Nchimbi alidai Februari 16, mwaka huu, katika Barabara ya Kawawa Mkwajuni, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, wakiwa wamekusanyika kutekeleza lengo la pamoja, waliendelea katika mkusanyiko huo na kufanya watu waogope kwamba watakwenda kusababisha uvunjifu wa amani.
Katika shtaka la pili la kuendelea na mkusanyiko usio halali, alidai Februari 16, mwaka huu katika Barabara ya Kawawa eneo la Mkwajuni, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, walikuwa wamekusanyika wao na wenzao 12 ambao hawajafikishwa mahakamani.
Alidaiwa kuwa watuhumiwa wakiwa kwenye maandamano na pasipo kuzingatia agizo lililotolewa na Ofisa wa Polisi, Gerald Ngiichi, waligoma na kuendelea na maandamano na kusababisha kifo cha Akwilina na majeruhi kwa askari wawili ambao ni H. 7856 PC Fikiri na E. 6976 CPL Rahim Msangi, ambao waliumia kutokana na mkusanyiko huo.
Shtaka la tatu, ambalo linamkabili mshtakiwa wa kwanza (Mbowe), ilidaiwa Februari 16, mwaka huu katika viwanja vya Buibui, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, Mbowe wakati akihutubia wananchi wa jimbo hilo alihamasisha chuki isivyo halali kwa kutoa matamshi yafuatayo:
“Ninapozungumza hapa kiongozi wetu wa Kata ya Kinondoni Hananasif yupo mochwari..amekamatwa na makada wa CCM kwa msaada wa vyombo vya ulinzi na usalama...wamemnyonga wamemuua. Halafu sisi tunaona ni jambo la kawaida...tunacheka na Polisi...tunacheka na CCM.”
Shtaka la nne ni uchochezi na kusababisha chuki miongoni mwa jamii ambapo inadaiwa Februari 16, mwaka huu, katika mkutano wa umma uliofanyika viwanja vya Buibui, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, Mbowe alifanya uchochezi na kusababisha chuki kinyume cha sheria kwa kutamka yafuatayo:
“Tumejipa kibali cha kutangulia mbele ya haki...haiwezekani wanaume wazima na akili zetu na wake zetu na watoto wetu tukafanywa ndondocha…hii ni nchi ya ajabu. Mimi leo nipo hapa kulinda taifa...
“Kule Afrika Kusini, Jacob Zuma, amelazimishwa kujiuzulu...Robert Mugabe wa Zimbabwe kang’olewa, kang’olewa Waziri Mkuu wa Ethiopia...juzi ameondoka kwa people's power. Magufuli ni mwepesi kama karatasi.”
Katika shtaka la tano la uchochezi wa uasi linalomkabili Mbowe, inadaiwa katika tarehe na maeneo hayo, alihutubia mkutano wa hadhara akiwa na nia ya kupandikiza chuki na dharau kwa Watanzania dhidi ya uongozi wa kisheria uliopo madarakani kwa kusema:
“Nitaongoza mapambano nchi hii kwa sababu tumechoka kuuawa...matokeo ya Watanzania mia watakaokufa wataleta haki katika taifa hili. Wangapi wapo tayari kuchukua bei hiyo?...”
Hata hivyo shtaka la sita la uchochezi wa uasi, Wakili Nchimbi aliendelea kudai, katika tarehe hiyo hiyo na maeneo hayo mkoani Dar es Salaam, Mbowe alitoa matamshi ya kupandikiza chuki na dharau kwa upande wa raia wa Tanzania dhidi ya mamlaka halali kuwa:
“Hii nchi inadharaulika...imejengewa misingi wa woga, kwa lugha nyingine wanaume ni kama mademu, si unawaona hao wanavaa suruali, waoga, bure kabisa...juzi ametekwa kijana wetu wanasema yupo mochwari, haki ya Mungu ingekuwa nchi nyingine Kinondoni ingekuwa majivu...
“Lissu amepigwa risasi, machine gun na vyombo vya dola...Watanzania mnarudi nyuma...kuna mwandishi wa habari leo ana siku 86 amebebwa na vyombo vya dola...suluhu ya nchi hii haipatikani bungeni…suluhu ya nchi hii ipo kwa wananchi wenyewe, lakini ili tupate suluhu hiyo…
“Ni lazima tukubali kubeba majeneza... Inawezekana leo mnaogopa kufa... Ni bora tuwabebe wachache hata wakiwa 200 waliokufa katika ukombozi ili hatimaye nchi hii isimame kama nchi ya wanaume wengine katika dunia hii.”
Katika shtaka la saba la kushawishi kutendeka kwa kosa la jinai, inadaiwa katika tarehe hiyo hiyo na maeneo hayo, Mbowe alishawishi wakazi wa Kinondoni kutenda kosa la kufanya maandamano na mkusanyiko usio halali.
Katika shtaka la nane la kushawishi utendaji wa kosa la jinai, linamkabili mshtakiwa wa pili, Msigwa, katika maeneo hayo hayo Msigwa anadaiwa kushawishi raia na wakazi wa eneo hilo kutenda kosa la jinai kwa kutembea mbele ya umma wakiwa na silaha.
Washtakiwa wote walikana mashtaka hayo na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika, hivyo wanaomba ipangwe leo au kesho kwa ajili ya kuwasomea maelezo ya awali.
Upande wa mashtaka uliiomba mahakama kuwasilisha maombi ya kunyimwa dhamana washtakiwa kwa njia ya mdomo.
Akiwasilisha sababu za kupinga dhamana hiyo, Dk. Mango alidai usalama wa jamii na nchi kiujumla hauko sawa iwapo washtakiwa watadhaminiwa.
Alidai kuwa wanatambua kupata dhamana ni haki ya mshtakiwa, lakini hakuna haki isiyokuwa na wajibu kwa mujibu wa Katiba ya nchi.
“Mashtaka yao yanaashiria kutokutii amri yao kikatiba, utekelezaji wa haki binafsi unapaswa kuzingatia haki za watu wengine,” alidai Mango.
Alidai makosa yanayowakabili yanahatarisha usalama na kuwapa dhamana ni kuendelea kuwapa nafasi ya kuendelea kufanya makosa hayo.
“Jukumu la dhamana liko chini ya mahakama hii, hata hivyo kabla ya mahakama kutumia mamlaka yake kutoa au kuzuia dhamana inapaswa kuangalia mazingira ya kosa husika,” alidai.
Aliiomba mahakama kuzingatia masilahi ya umma kwa ujumla wake kwa hatari ya makosa wanayoshtakiwa nayo na usalama wa taifa.
Wakili Nchimbi alidai kuwa kama washtakiwa wataruhusiwa kurudi uraiani baada ya matamko hayo ni wazi kwamba haki ya upande wa pili itapotea.
“Matamshi hayo yana madhara endelevu kwa Watanzania, kwani tuna taarifa za upelelezi kwamba baadhi ya mambo yaliyoongelewa, ushawishi uliotolewa unaonekana, kuna utekelezaji wa kihalifu,” alidai.
Wakili Nchimbi aliiomba mahakama itoe amri ya kuzuia dhamana.
No comments:
Post a Comment