WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imetenga sh. bilioni 4.3 ili kujenga vituo vya kuhifadhi damu (satellite blood banks) kwenye mikoa 12.
Ameitaja
mikoa hiyo kuwa ni Manyara, Katavi, Rukwa, Ruvuma na Njombe. Mingine ni
Tanga, Arusha, Pwani, Singida, Songwe, Geita na Simiyu.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Juni 29, 2018) bungeni jijini Dodoma katika hotuba yake aliyoitoa wakati wa kuahirisha Mkutano wa 11 wa Bunge.Bunge limeahirishwa hadi Septemba 4, mwaka huu.
Amesema
lengo la mpango huo ni kuboresha upatikanaji wa damu hasa kwa akinamama
wanaopoteza damu nyingi wakati wa kujifungua. “Serikali imedhamiria
kupunguza vifo vya akinamama na watoto vitokanavyo na uzazi. Katika
kutekeleza azma hiyo, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo
inaendelea kufanya ukarabati na ujenzi wa majengo ya upasuaji, maabara,
wodi za wazazi, nyumba za watumishi na wodi za watoto,” amesema.
Amesema
kukamilika kwa majengo hayo, kutaboresha huduma za uzazi kwa akinamama
na watoto wachanga. “Hatua hii itawezesha upatikanaji wa huduma kamili
za uzazi na kupunguza vifo vya mama na watoto. Katika mwaka 2018/2019,
eneo litakalopewa kipaumbele ni kuimarisha upatikanaji vifaa na
watumishi katika vituo 208 vinavyoendelea kuboreshwa,” amesema.
Waziri
Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasihi watumishi wa afya, waongeze juhudi ya
kuhamasisha wananchi wajitolee damu na pia akawaomba wananchi nao wawe
na utamaduni wa kuchangia damu ili kuwezesha upatikanaji wa damu salama
itakayohifadhiwa kwenye benki hizo.
Wakati huohuo, Waziri
Mkuu amesema Serikali inaendelea kuimarisha huduma za kibingwa nchini
kwa kutenga shilingi bilioni 14 ili kuanzisha huduma ya kuchunguza mwili
bila upasuaji (PET Scan) katika taasisi ya Saratani ya Ocean Road.
Amesema
kuanza kwa huduma hiyo kutapunguza asilimia 80 ya wagonjwa wa saratani
waliokuwa wanapelekwa nje ya nchi kwa ajili ya kipimo hicho na kwamba
Serikali itaweza takribani shilingi bilioni 5 kwa mwaka zilizokuwa
zinatumika kwa ajili ya kulipia wagonjwa waliokuwa wakienda nje ya nchi
kwa ajili ya kipimo hiki.
Amesema
Serikali itasogeza huduma ya tiba ya saratani katika ngazi ya Hospitali
za Kanda ikiwa ni pamoja na Hospitali ya Bugando Mwanza, Hospitali ya
Kanda ya Kaskazini KCMC na Hospitali ya Rufaa ya Kanda za Nyanda za Juu
Kusini, jijini Mbeya.
“Vilevile,
katika mwaka 2018/2019, Serikali itaimarisha upatikanaji wa huduma za
kibingwa katika hospitali za rufaa za mikoa kwa kuboresha miundombinu ya
kutolea huduma za afya ikiwa ni pamoja na majengo, vifaa tiba na
madaktari bingwa. Jumla ya shilingi bilioni 40 zimetengwa kwa ajili ya
kuimarisha hospitali hizi,” amesema.
Katika hatua nyingine,
Waziri Mkuu amesema Serikali kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo
kupitia Mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo (Education Performance for
Results - EP4R) itaimarisha miundombinu kwenye shule zenye uhitaji
mkubwa.
“Katika
mwaka 2018/2019, Serikali itatumia shilingi bilioni 155.58 kwa ajili ya
ukarabati wa shule kongwe 25, ununuzi wa vifaa vya maabara, ujenzi wa
mabwalo 85, vyumba vya madarasa 2,000 na motisha kwa Halmashauri
kutokana na ufanisi katika utekelezaji wa vigezo vya EP4R,” amesema.
Amesema
kwa sasa, Serikali inatarajia kuajiri walimu 4,785 wa shule za msingi
zenye uhitaji mkubwa na kwamba tayari imeshatangaza nafasi za ajira kwa
walimu 2,000 wa masomo ya sayansi, hisabati na lugha ambao watapangwa
kwenye shule za sekondari zenye uhitaji mkubwa.
Amesema
kuwa Serikali imetangaza nafasi za ajira kwa mafundi sanifu maabara 160
ambao nao pia watapangwa kwenye shule zenye uhaba wa wataalamu hao.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 - DODOMA.
IJUMAA, JUNI 29, 2018.
No comments:
Post a Comment