WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amempokea Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea, Lee Nak-yon ambaye amewasili nchini leo saa 12:30 jioni (Jumamosi, Julai 21, 2018) kwa ziara ya kikazi ya siku tatu.
Kwenye uwanja wa ndege, Waziri Mkuu huyo wa Jamhuri
ya Korea alipokelewa pia na Waziri wa Mambo ya Nje, Dk. Augustine Mahiga, Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Isack Kamwele, Waziri wa Nishati, Dk.
Medard Kalemani, Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Eng. Stella
Manyanya na viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam.
Waziri Mkuu Lee Nak-yon anatembelea Tanzania ikiwa
ni hatua ya kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizi mbili. Hii
ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa ngazi ya juu wa nchi hiyo kufanya ziara ya
kiserikali tangu nchi hizo zianzishe mahusiano ya kidiplomasia mwaka 1992.
Pia ameambatana na ujumbe wa maafisa wa Serikali,
wabunge na wafanyabiashara wakubwa ambao watashiriki Kongamano la Kibiashara baina
ya Korea na Tanzania (Korea-Tanzania Business Forum) lililopangwa kufanyika
kesho kutwa (Jumatatu, Julai 23, 2018) kwenye hoteli ya Serena, jijini Dar es
Salaam.
Kesho (Jumapili, Julai 22, 2018), Waziri Mkuu Lee Nak
Yon atakuwa na mazungumzo rasmi ya kiserikali na mwenyeji wake pamoja na
viongozi kadhaa wa Serikali na pia kwa pamoja watashuhudia uwekaji saini
mkataba wa kuondoa hitaji la viza kwa watu wenye hati za kusafiria za
kidiplomasia na za utumishi (diplomatic and service passports).
Pia ataenda Ikulu kumsalimia Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, atatembelea Makumbusho ya
Taifa, Hospitali ya Mnazi Mmoja na kituo cha utunzaji taarifa cha NIDA kilichopo
Kibaha.
Anatarajiwa
kuondoka nchini Jumatatu jioni, Julai 23, 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimina na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea , Lee Nak -Yon wakati mgeni huyo alipowasili kwenye ukumbi wa Kikwete, Ikulu jijini Dar es salaam kwa mazungumzo rasmi ya kiserikali, Julai 22, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimina na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea , Lee Nak -Yon wakati mgeni huyo alipowasili kwenye ukumbi wa Kikwete, Ikulu jijini Dar es salaam kwa mazungumzo rasmi ya kiserikali, Julai 22, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mgeni wake, Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Korea, Lee Nak - Yon (kushoto ) wakiwa katika
mazungumzo rasmi ya kiserikali kwenye ukumbi wa Kikwete, Ikulu jijini
Dar es salaam Julai 22, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea, Lee
Nak - Yon (kushoto) wakishuhudia wakati Waziri wa Mambo ya Nje, Dkt.
Augustine Mahiga na Makamu wa Kwanza wa Wizara ya Mambo ya Nje ya
Jamhuri ya Korea, Lim Sung - Nam (kushoto) walipotia saini Mkataba wa
kuondoa Hitaji la Viza za Kusafiria kwa Watu Wenye Hati za Kusafiria za
Kidiplomasia na Kikazi, kwenye ukumbi wa Kikwete, Ikulu jijini Dar es
salaam Julai 22, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
No comments:
Post a Comment