Na Benny Mwaipaja, WFM, Mtwara
WAZIRI wa
Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ameuahidi uongozi wa Kituo cha
Utafiti wa Kilimo Naliendele kwamba Serikali itakiwezesha Kituo hicho na
vituo vingine vya utafiti nchini ili viendeleze kazi ya utafiti wa
mazao ya kilimo ambacho kinategemewa na watanzania wengi katika
kujikwamua kiuchumi.
Dkt. Mpango ametoa ahadi
hiyo alipotembelea Kituo cha Utafiti Naliendele, mkoani Mtwara, ambacho
uongozi wake ulielezea wasiwasi wake wa kupata rasilimali fedha za
kuendeleza utafiti wa mazao likiwemo zao la korosho pamoja na watumishi
baada ya kuondolewa kwa fedha za ushuru wa korosho inayouzwa nje,
zilizokuwa zikitumika kuendeleza utafiti huo.
Alisema
kuwa Serikali inatambua umuhimu wa shughuli za utafiti katika
kuendeleza uchumi na maendeleo ya nchi kwa ujumla na kwamba atajitahidi
kama Waziri wa Fedha na Mipango kwa kushirikiana na Waziri mwenzake
anayeshughulikia kilimo ili taasisi hiyo isikwame kufanya shughuli zake.
"Niwahakikishie
kabisa kwamba Serikali haitakubali utafiti wa mazao yote unaofanyika
hapa likiwemo zao la korosho udhurike, litakuwa ni janga kubwa, kwahiyo
upatikanaji wa fedha za Kituo hiki litakuwa ni moja ya vipaumbele
vyangu" alisisitiza Dkt. Mpango.
Alisema kuwa
kilimo ndiyo uti wa mgongo wa Taifa na kwamba hakutakuwa na mapinduzi ya
viwanda bila kilimo kwa sababu viwanda vinavyojengwa vinatarajiwa
kuongeza thamani ya mazo ya kilimo pamoja na mazao ya mifugo na uvuvi.
Pause: Dkt. Philip Mpango -Waziri wa Fedha na Mipango
Awali,
Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo Naliendele, Dkt. Omari
Mponda, alieleza kuwa Kituo chake kinahitaji zaidi ya shilingi bilioni 7
kwa mwaka ili kiweze kuendeleza shughuli za utafiti hasa baadaya
Serikali kuamua kupanua shughuli za utafiti wa zao la korosho kwenye
mikoa mingine nchini.
Alisema kuwa hivi sasa
Kituo kimeelekeza nguvu zake katika utafiti wa ugonjwa mpya unaoathiri
kwa kiwango kikubwa zao la korosho ujulikanao kama mnyauko fusari
(Fusarium wilt) , ulioathiri zao hilo katika maeneo mbalimbali nchini
ikiwemo Mkuranga, Masasi, Tandahimba, Mtwara na Liwale, lakini
changamoto kubwa inayowakumba ni ukosefu wa fedha za kuendeleza utafiti
huo.
"Mheshimiwa Waziri, Kituo hiki pia kina
zaidi ya asilimia 50 ya watumishi ambao wameajiriwa kwa njia ya mikataba
na wanahitaji kulipwa vizuri ili wabaki Kituoni hapa kuendeleza
shughuli za utafiti ndio maana nasema tuna mahitaji makubwa ya fedha na
tunaiomba Serikali iliangalie jambo hili" Alisema Dkt. Mponda.
Pause: Dkt. Omari Mponda -Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti Naliendele
Kituo cha
Utafiti Naliendele kilichoko mkoani Mtwara kinatajwa kuwa ni kitovu cha
utaalamu wa zao la korosho katika Bara la Afrika na kwamba tafiti
nyingi, ikiwemo aina 54 za mbegu za zao la korosho kunakifanya kituo hicho kuwa
tegemeo kwa masuala ya utafiti katika nchi nyingi za afrika ambazo
hutumia Taasisi hiyo kupata teknolojia ya uzalishaji wa mbegu bora za
mazao mbalimbali hususan korosho.
No comments:
Post a Comment