WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemtembelea na kumpa pole Waziri wa Maliasili na
Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla ambaye amelazwa katika Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili (MNH) akipatiwa matibabu baada ya kupata ajali.
Akiwa hospitalini hapo leo (Jumapili, Agosti 5, 2018), Waziri Mkuu ambaye ameambatana na mkewe Mama Mary Majaliwa amesema amefarijika baada ya kumkuta Dkt. Kigwangalla na wagonjwa wengine waliolazwa katika hospitali hiyo wakihudumiwa vizuri.
“Hospitali
ya Muhimbili ndio kimbilio letu kwa sasa na tunawashukuru madaktari na
wauguzi kwa kazi nzuri mnayoifanya ambayo inaliletea heshima Taifa letu
kwani hata watu wa Comoro wanakuja kutibiwa Muhimbili,” amesema.
Kwa upande wakeDkt.
Kigwangalla amesema anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa sababu ajali ilikuwa
mbaya sana. “Ajali ilikuwa mbaya sana hivi sasa naongea hapa namshukuru
Mungu, Serikali pamoja na madaktari na wauguzi kwa jitihada kubwa
walizozifanya,”.
Dkt.
Kigwangalla alipata ajali jana asubuhi (Jumamosi, Agosti 4, 2018)
katikati ya vijiji vya Mdolii na Minjingu wilaya ya Babati mkoani
Manyara baada ya gari lake kupinduka na kusababisha kifo cha Afisa
Habari wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. Hamza Temba na wengine
watano akiwemo Dkt. Kigwangalla kujeruhiwa.
Pia
Waziri Mkuu amjulia hali msanii maarufu wa maigizo nchini, Bw. Amri
Athumani maarufu King Majuto ambaye amelazwa katika Hospitali ya Taifa
ya Muhimbili akipatiwa matibabu. Amesema amefarijika kumkuta akiwa
anaendelea vizuri.
Naye
Mzee Majuto amesema anaishukuru Serikali kwa sababu inamuhudumia
vizuri. “Mheshimiwa nakushukuru sana na naishukuru Serikali kwani hata
sijui ingekuwaje kama si msaada wa Serikali. Hii ni bahati kubwa,”.
Pia
Waziri Mkuu amemjulia hali Bibi Hellena Baruti ambaye ni mama mzazi wa
Mthamini Mkuu wa Serikali Bibi Evelyne Mugasha aliyelazwa katika Taasisi
ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) akipatiwa matibabu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, AGOSTI 5, 2018.
No comments:
Post a Comment