HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 25, 2018

NMB KUCHOCHEA UCHUMI WA VIWANDA TANZANIA


Mkuu wa Idara ya Wateja Wakubwa na Serikali wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi (kushoto) akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dodoma jana kwenye Mkutano Mkuu wa 34 wa Jumuiya ya Tawala za Mikoa (ALAT) unaoendelea Jijini hapo. Mkutano huo unaoshirikisha zaidi ya washiriki 500 kutoka Halmashauri, Wizara na Idara mbalimbali za Serikali umedhaminiwa na benki hiyo.

Meneja wa Kanda ya Kati wa Benki ya NMB, Nsolo Mlozi akizungumza na Waandishi Habari Jijini Dodoma jana kwenye mkutano mkuu wa 34 wa Jumuiya ya Tawala za Mikoa (ALAT) unaoendelea Jijini hapo, Mkutano huo unawashirikisha washiriki zaidi ya 500 kutoka Halmashauri, Wizara na Idara mbalimbali za Serikali umedhaminiwa na benki hiyo.

Baadhi ya Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 34 wa Jumuiya ya Tawala za Mikoa (ALAT) wakipata maelezo walipotembelea banda la Maonesho la Benki ya NMB Ukumbi wa Dr. Jakaya Kikwete Jijini Dodoma jana- mkutano huo umedhaminiwa na benki ya NMB. 

Dodoma, Septemba 25, 2018
 
BENKI ya NMB Plc imesema itaendelea kusaidia jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kukuza uchumi wa viwanda nchini Tanzania.
 
Akizungumza na vyombo vya habari jana katika mkutano mkuu wa 34 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) unaoendelea jijini Dodoma, Mkuu wa Idara ya Wateja Wakubwa na Serikali wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi, amesema benki yake imetengeneza program mbalimbali za kusaidia kuchochea kasi ya uchumi wa viwanda nchini Tanzania.

Hata hivyo, amesema, benki ya NMB ambayo inamilikiwa na Serikali kwa asilimia 31, ni miongoni mwa taasisi chache za fedha hapa nchini zinazofanya kazi kwa ukaribu sana na Serikali.

“Kwa mfano, NMB imekuwa mdhamini mkuu wa mikutano mikuu ya ALAT miaka sita sasa, na kwa mwaka huu, benki imetoa udhamini wa shilingi milioni 100. Hii inaonyesha utayari wetu katika kufanya kazi pamoja na Serikali,” alisema.

Aidha, amesema NMB inafanya kazi pamoja na wilaya na halmashauri zote nchini, ikiwa ni pamoja na kutoa mikopo rafiki kwa wafanyakazi wa Serikali.

“Lengo ni kuhakikisha huduma za kifedha za NMB zinawafikia Watanzania wote nchini hususani wale wanaoishi katika jamii za vijijini ambapo kunachangamoto nyingi za kimaisha na kiuchumi,” alieleza.

Amesema kwa sasa benki imetenga kiasi cha shilingi bilioni 500 kwa ajili ya kutoa mikopo rafiki kwa wajasiliamali wa kati na wadogo nchini, lengo kuu likiwa ni kuchochea uchumi wa viwanda kupitia sekta ya kilimo na mifugo.

“Uchumi wa viwanda unategemea sana sekta ya kilimo na mifugo na hivyo, NMB itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kuwasaidia wajasiliamali wadogo wadogo kupata mikopo nafuu na rafiki ili waweze kujikita katika miradi husika,” aliongeza.

Pamoja na hayo, amesema ili kuhakikisha wajasiliamali wanufaika wa mikopo ya NMB wanafikia malengo yao, benki imefungua vilabu vya biashara nchi nzima, ili kutoa mafunzo maalumu ya mipango biashara.

“Kutokana na usimamizi na utendaji mzuri wa benki ya NMB, tumefanikiwa kutoa kiasi cha shilingi bilioni 98 kama gawio kwa Serikali katika kipindi cha miaka saba iliyopita (2010 -2017),” aliongeza.

Mponzi aliongeza kuwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, benki imetumia zaidi ya shilingi bilioni 280 kutoa mikopo mbalimbali kwa wakulima na wachakataji wa mazao mbalimbali hapa nchini.
 
Kwa upande wake, Meneja wa NMB Kanda ya Kati, Msolo Mlozi, amesema benki imejipanga vyema kusaidia maendeleo ya sekta mbalimbali katika kanda ya kati, hususani kipindi hiki ambacho Serikali imehamishia makao yake makuu rasmi jijini Dodoma.
 
“Baada ya Serikali kuhamia jijini Dodoma kumekuwa na ongezeko kubwa la watu, hali ambayo imepelekea pia ongezeko kubwa la mahitaji mengi ambayo yanahitaji huduma bora na karibu za kifedha. NMB itaendelea kuboresha huduma zake katika kanda ya kati ili kuchochea kasi ya maendeleo pamoja na kutoa huduma nzuri zaidi kwa wateja wake,” alieleza.
 
Mlozi ameitaja baadhi ya mikakati ya benki hiyo katika kanda ya kati kuwa ni pamoja na kusaidia wakulima wa alizeti, zabibu na mahindi, pamoja na kutoa mikopo mingine rafiki kwa wajasiliamali.
Baadhi ya Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 34 wa Jumuiya ya Tawala za Mikoa (ALAT) wakipata maelezo walipotembelea banda la Maonesho la Benki ya NMB Ukumbi wa Dr. Jakaya Kikwete Jijini Dodoma jana- mkutano huo umedhaminiwa na benki ya NMB.

Wajumbe wa Mkutano Mkutano Mkuu wa 34 wa Jumuiya ya Tawala za Mikoa (ALAT) wakishiriki mkutano huo ndani ya ukumbi wa mikutano wa Dr. Jakaya Kikwete Jijini Dodoma- mkutano huo umedhaminiwa na Benki ya NMB.

No comments:

Post a Comment

Pages