Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George H.
Mkuchika (Mb) akizungumza na wananchi na wanufaika wa TASAF, kijiji cha
Kitagata Wilayani Kasulu alipowatembelea ili kujionea utekelezaji wa Mpango wa
Kunusuru Kaya Maskini nchini.
Baadhi ya
wanakijiji na wanufaika wa TASAF wa kijiji cha Kitagata Wilayani Kasulu
wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst)
George H. Mkuchika (Mb) (hayupo pichani) alipotembelea kijiji hicho ili
kujionea utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George H. Mkuchika (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na watoto wa kijiji cha Kitagata Wilayani Kasulu ambao ni watoto wa mnufaika wa TASAF alipokitembelea kijiji hicho ili kujionea utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini.
Wanufaika wa Mpango
wa Kunusuru Kaya Maskini Kijiji cha Kitagata Wilayani Kasulu wamepongezwa kwa mafanikio
waliyoyapata katika utekelezaji wa mpango wa TASAF na kwa kutoa rambirambi ya
chakula kwa wahanga waliopotelewa na ndugu, jamaa na marafiki kutokana na ajali
ya kuzama kwa kivuko cha MV. Nyerere iliyotokea Septemba 20, 2018.
Pongezi hizo
zimetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst)
George H. Mkuchika (Mb) wakati akizungumza na wananchi na wanufaika wa
Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika kijiji cha Kitagata alipowatembelea wanufaika
hao kwa lengo la kujionea utekelezaji wa mpango huo.
Mhe. Mkuchika amesema
kuwa, wanufaika hao wametumia vizuri fedha za ruzuku kwa kununua vitu
mbalimbali ikiwamo vifaa vya shule vya watoto wao, chakula cha familia, bati za
kuezekea nyumba zao pamoja na kujenga nyumba bora za kuishi, kufuga na kujiunga
na bima ya afya.
Mhe. Mkuchika amesisitiza
kuwa, mradi wa TASAF lengo lake ni kupambana na umaskini kwa watanzania wote
wanaostahili kunufaika na Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini, na kuongeza
kuwa, awamu ya tatu ya TASAF imelenga kumuwezesha mwananchi mmoja mmoja tofauti
na ilivyokuwa katika TASAF awamu ya kwanza na ya pili ambayo ililenga kujenga
zahanati, kutengeneza barabara, kujenga madarasa, vyoo, shule na nyumba za
walimu.
Mhe. Mkuchika amefafanua
kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
anataka ndani ya kipindi cha miaka miwili ijayo, watanzania wote ambao hawana
uwezo kiuchumi wawezeshwe kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.
Aidha, Mhe.
Mkuchika amewapongeza wanufaika wa TASAF katika kijiji cha Kitagata wilayani
Kasulu kwa kuguswa na maafa yaliyotokana na kuzama kwa kivuko cha MV. Nyerere
kisiwani Ukerewe, hivyo kutoa rambirambi ya magunia saba ya chakula aina ya
muhogo kwa wahanga wa ajali hiyo.
Mhe. Mkuchika anaendelea
na ziara ya kikazi mkoani Kigoma yenye lengo la kuangalia utekelezaji wa Mpango
wa Kunusuru Kaya Maskini nchini, ambapo mpaka sasa ameshawatembelea wanufaika katika
Manispaa ya Kigoma Ujiji, Halmashauri ya Mji wa Kasulu na Halmashauri ya Wilaya
ya Kasulu, ikiwa ni pamoja na kukutana na watumishi wa umma katika Sekretarieti
ya Mkoa wa Kigoma, Manispaa ya Kigoma Ujiji, Halmashauri ya Mji wa Kasulu na
Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji na kuboresha
Utumishi wa Umma nchini.
IMETOLEWA NA:
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
OFISI YA RAIS (UTUMISHI)
TAREHE 25 SEPTEMBA,
2018
No comments:
Post a Comment