*Awataka
Watanzania waiache Serikali na dola vifanye kazi yake
*Asema
tume ya uchunguzi itatangazwa karibuni, wahusika kuchukuliwa hatua
*Waziri
Mhagama atangaza namba ya tigopesa kupokea michango
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameongoza maelfu ya wakazi wa wilaya ya Ukerewe
mkoani Mwanza na mkoa jirani wa Mara katika mazishi ya kitaifa ya watu waliopoteza maisha kwenye ajali ya MV Nyerere
Septemba 20, mwaka huu.
Waziri Mkuu ambaye ameongoza mazishi hayo leo (Jumapili,
Septemba 23, 2018) kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.
John Pombe Magufuli, amewataka Watanzania waiache Serikali na vyombo vya dola
viendelee kufanya kazi yake.
“Wito wa Serikali kwenu wote, ni kuwasihi
tushikamane na wenzetu waliopoteza ndugu zao, wakiwemo wazazi, kaka, dada na
watoto. Ninaomba tuiache Serikali na vyombo vya dola viendelee kufanya kazi
yake. Tuendelee kuwa wavumilivu,” amesema.
Akiwasilisha salamu za rambirambi
kutoka kwa Rais Magufuli mbele
ya wafiwa na waombolezaji, Waziri Mkuu amesema: “Mheshimiwa Rais alipokea tukio
hili kwa mshtuko mkubwa na anawapa pole sana wafiwa wote pia anawaombea
majeruhi wote wapate ahueni mapema.”
Amesema jumla ya watu 224 walipoteza maisha
kutokana na ajali hiyo. Kati ya hao, miili 214 kati ya 219 iliyotambuliwa, ilichukuliwa
na ndugu zao. Miili minne haikuweza kutambuliwa lakini ipo miili mitano ambayo
ilitambuliwa na ndugu zao na hao ndugu wakaona ni vema wazikwe hapa eneo la
tukio. Kwa hiyo leo tutawazika ndugu zetu tisa katika eneo hili,” amesema.
Waziri Mkuu amesema Serikali imechukua hatua
ya kuunda tume ya uchunguzi na kuahidi kwamba tume hiyo itatangazwa wakati
wowote. “Tume ikikamilisha kazi yake, wote watakaobainika kuwa wamehusika
watachukuliwa hatua mara moja,” amesema.
Ili kukabiliana na tatizo la usafiri lililopo,
Waziri Mkuu amesema meli ya MV Nyehunge imeanza kutoa huduma ya usafiri wa muda
badala ya MV Nyerere iliyokuwa ikitoa huduma kati ya bandari ndogo ya Bugolora,
Ukerewe na kisiwa kidogo cha Ukara.
Amesema jitihada za kuivuta meli ya MV Nyerere
iliyopinduka zinaendelea na kwamba maafisa wote wanaohusika na usafiri wa
majini ambao walizembea kwenye suala hilo, wamekamatwa na wameanza kuhojiwa.
Akigusia chanzo cha ajali hiyo, Waziri Mkuu
amesema inasadikiwa kivuko cha MV Nyerere kilibeba mizigo mingi kuliko uwezo
wake ambao ni wa kubeba tani 25 za mizigo, magari matatu na abiria 101. “Hadi
sasa inaonesha kulikuwa na watu zaidi ya 260, yaani 41 waliookolewa na 224
waliopoteza maisha,” amesema.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwashukuru
wananchi wote wa Ukara waliojitokeza kusaidia kazi ya uokoaji tangu ajali hiyo
ilipotokea. Pia aliwashukuru wote waliotoa michango mbalimbali, watumishi wa
hospitali za Bugando, Sekou Toure, Ukerewe, kituo cha afya cha Bwisya na timu
nzima inayofanya kazi ya uokoaji na uopoaji wa miili kwa kazi kubwa
waliyoifanya.
Wakati huohuo, Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenista Mhagama
ametangaza namba ya tigopesa ambayo wananchi wanaweza kuitumia kutuma michango
yao kwa ajili ya waliopatwa na maafa hayo.
“Tumefungua akaunti ya maafa kwenye Benki ya
NMB tawi la Kenyatta lakini ili kurahisisha upokeaji wa michango kutoka kwa
wananchi wa kawaida, tumesajili namba ya tigo yenye namba 0677-030-000 kwa jina
la RAS Mwanza. Naomba wale wasioweza kwenda benki watumie namba hiyo,” amesema.
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI,
SEPTEMBA 23, 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiweka shada la maua kwenye
kaburi la mmoja wa wananchi walifariki katika ajali ya kivuko cha MV
Nyerere kilichozama katika katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe.
Majaliwa aliwaongoza mamia ya waombolezaji katika mazishi yaliyofanyika
kwenye kijiji hicho Septemba 23, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitoa heshima kwenye kaburi la
mmoja wa wananchi walifariki katika ajali ya kivuko cha MV Nyerere
kilichozama katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe. Majaliwa
aliwaongoza mamia ya waombolezaji katika mazishi yaliyofanyika kwenye
kijiji hicho Septemba 23, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapa pole wafiwa katika
mazishi ya mwananchi waliofariki katika ajali ya Kivuko cha MV Nyerere
kilichozama katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe. Majaliwa
aliwaongoza mamia ya waombolezaji katika mazishi yaliyofanyika kwenye
kijiji cha Bwisa kisiwani Ukara Septemba 23, 2018. (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapa pole wafiwa katika
mazishi ya mwananchi waliofariki katika ajali ya Kivuko cha MV Nyerere
kilichozama katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe. Majaliwa
aliwaongoza mamia ya waombolezaji katika mazishi yaliyofanyika kwenye
kijiji cha Bwisa kisiwani Ukara Septemba 23, 2018. (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa akipewa maelezo na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella kuhusu
juhudi zinazofanywa na wahandishi za kukivuta kivuko cha MV Nyerere
kilichozama katika Kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe wakati aliposhiriki
katika mazishi ya wananchi waliokufa katika ajali ya kivuko hicho
kwenye kijiji cha Bwisa kisiwani Ukara Septemba 23, 2018. (Picha na
Ofisi ya Waziri Mkuu)
Askofu wa
Jimbo Katoliki la Bunda, Renatus Nkwande akiomba katika mazishi ya
wananchi waliofariki dunia katika ajali ya Kivuko cha MV Nyerere
kilichozama katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe. Mazishi hayo
yaliyoongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa yalifanyika katika kijiji
cha Bwisa kisiwani Bukara, Septemba 23, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu)
No comments:
Post a Comment