*Asisitiza kwamba vitendo hivyo vinawadharirisha
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewaonya maafisa elimu na walimu kutojihusisha na vitendo vya wizi wa
mitihani vinavyofanywa kwa lengo la kuwasaidia wanafunzi kwa sababu
vinawadharirisha.
“Kama
kweli umemuandaa mtoto huna sababu ya kuiba mitihani na mtoto hawezi
kufikiria kuiba mitihani kwa sababu yuko nje ya mfumo. Walimu heshimuni
maadili ya kazi ya ualimu.”
Waziri Mkuu ametoa onyo hilo leo (Jumanne, Oktoba 9, 2018) baada ya kukabidhiwa vyumba vya madarasa vya shule za msingi Nyakato na Kashozi, wilayani Bukoba.
Vyumba
hivyo vilivyojengwa kwa msaada wa Serikali ya Japan baada ya kuathiriwa
na tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera mwaka 2016.
Waziri
Mkuu amesema tathmini ya elimu katika shule za msingi na sekondari
hufanyika kwa kufanya mitihani, dosari ya udanganyifu wa mitihani
iliyojitokeza katika mitihani ya darasa la saba mwaka huu isijirudie
tena.
Wiki
iliyopitaBaraza la Mitihani la Taifa (NECTA) lilifuta matokeo ya
mitihani ya darasa la saba kwa shule za msingi zote za Halmashauri ya
Chemba na baadhi ya shule katika halmashauri ya Kondoa, Kinondoni,
Mwanza jiji na Ubungo kwa kosa la kuvujisha mitihani.
Waziri
Mkuu amesema tayari Serikali imechukua hatua kali kwa watu wote
walioshiriki katika kitendo hicho kwa sababu kinadumaza uelewa na
ufikiri kwa wanafunzi, hivyo kuwaandaa watoto kuwa wategemezi.
“Hata hivyo, Serikali inaendelea na uchunguzi juu ya suala hili ili kubaini chanzo cha wizi huo. Walimu,
kitendo cha kumpa mtoto mitihani ni sawa na kujiaibisha kwani
mnaonekana hamjafanya kazi zenu ipasavyo. Sitarajii kusikia suala hili
tena.”
Katika hatua nyingine,
Waziri Mkuu ametembelea kiwanda cha kahawa cha Amimza ambacho ni kati
ya viwanda vikubwa vitano vya kusindika kahawa Barani Afrika, ambapo
ametumia fursa hiyo kumpongeza mwekezaji mzawa Bw. Amiri Hamza na
kumuhamasisha aongeze uzalishaji.
Kadhalika,
Waziri Mkuu ametembelea kituo cha utafiti Maruku ambapo alikagua na
kupokea taarifa za shughuli za utafiti wa zao la kahawa na alitumia
fursa hiyo kuwashauri wakulima wenye miti mikongwe kung’oa na kupanda
mipya kwa awamu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, OKTOBA 9, 2018.
No comments:
Post a Comment