HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 03, 2018

WAZIRI MKUU AWASAIDIA WATOTO WENYE ULEMAVU

*Ataka uongozi wa Jiji la Dodoma utembelee vituo vyote vya watoto wa aina hiyo

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa msaada wa vyakula na mahitaji mengine kwa watoto wenye ulemavu wa akili wenye thamani ya sh. 2,359,000.

Alikabidhi msaada huo jana jioni (Jumanne, Oktoba 3, 2018) mbele ya uongozi wa kituo cha Miyuji Cheshire Home kilichopo nje kidogo ya jiji la Dodoma wakiwemo wajumbe wa Bodi, walimu na walezi.

Vifaa hivyo ni mchele kilo 200, dengu (kg. 100), choroko (kg.30), mafuta ya kula (lita 40), sabuni ya mche katoni moja, asali (lita 20). Vingine ni sukari (kg. 51), maji katoni sita, juisi katoni mbili, majani ya chai katoni moja, kahawa na fedha taslimu sh. 226,000/-.

Akizungumza mara baada ya kukagua majengo na miradi ya shamba la zabibu, ufugaji na bustani ya kituo hicho, Waziri Mkuu alisema ameguswa sana na moyo wa kujituma unaooneshwa na masista, walimu na walezi kwa watoto wanaolelewa kwenye kituo hicho.

“Kazi ya kuwatunza hawa watoto ni kubwa sana inayohitaji upendo, moyo wa huruma na uvumilivu. Mimi nimekaa nao kwa dakika chache tu, kazi nimeiona, kwa kweli mnastahili pongezi sana,” amesema.

Alisema amefurahi kusikia kwamba watoto 442 walipatiwa fursa ya kulelewa kwenye kituo hicho na kusisitiza kwamba Serikali ya awamu ya tano imewaagiza watendaji wa vijiji wahakikishe watoto wenye ulemavu wanapelekwa shule.

“Tumetoa maelekezo kwa watendaji wa vijiji wafanye msako na kuwasisitiza wazazi wawatoe nje watoto wao wenye ulemavu na kuwapeleka shule. Tumegundua kuwa hawa watoto wakipelekwa shule wanafanya vizuri sana,” alisema.

Kuhusu changamoto ya uhaba wa walimu na wataalamu kwenye kituo hicho, Waziri Mkuu alisema jukumu la msingi la kusimamia masuala ya walemavu ni la Halmashauri. Amewataka Afisa Elimu wa Jiji la Dodoma na Mkurugenzi wa Elimu (TAMISEMI) watembelee vituo vyote vya mkoa huo vyenye watoto wenye mahitaji maalum na kuainisha changamoto zinazowakabili na wazitafutie ufumbuzi.

“Afisa Elimu wa Jiji na Mkurugenzi wa Elimu Maalum pale TAMISEMI wakae na kufanya tathmini ya hali ilivyo ili walimu wenye taaluma hii waletwe hapa kujaza mapengo yaliyopo,” alisema.

“Suala la wataalamu wa physiotherapy na speech therapy itabidi Naibu Waziri Mavunde afuatilie Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuona watapatikanaje,” alisema.

Mapema, akitoa taarifa ya kituo hicho, Mkuu wa kituo cha Miyuji Cheshire Home, Sista Bertha Ligoha alisema kituo hicho chenye uwezo wa kutunza watoto 40, hivi sasa kina watoto 28 ambao kati yao 19 ni wa kiume na tisa ni wa kike.

Alisema kituo hicho kilichoanzishwa mwaka 1987, kimeshapokea watoto 442 ambao kati yao 165 ni wa kike na 477 ni wa kiume. Alisema hivi sasa kituo kina walimu wawili tu (mmoja yupo na mwingine yuko masomoni) na kinahitaji walimu sita zaidi.

Aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuwapatia vitanda 40 na pia wabunge na Mawaziri ambao walichanga fedha na kuwanunulia magodoro 80.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya kituo hicho, Bw. Peter Mavunde alisema wanakabiliwa na changamoto nyingine zikiwemo ukosefu wa vyanzo vya uhakika vya mapato vya kuendeshea kituo hicho, upungufu wa walimu na ukosefu wa gari la kupeleka watoto kwenye matibabu pindi wanapozidiwa.

“Tunakabiliwa na changamoto kubwa ya kupata fedha za kuwalipa wahudumu na walezi. Tulipoingia tulikuta wanalipwa sh.45,000 kwa mwezi, tukajipigapiga hadi wakaweza kulipwa sh. 60,000 kwa mwezi. Tunatamani tufikishe kiwango cha sh. 100,000 lakini hali ni ngumu kwetu,” alisema.

Alisema wanahitaji pia vifaa vya mazoezi kwa watoto hao na kuongeza kuwa wana shida ya kupata ulinzi wa eneo la kituo hicho kwa sababu makampuni ya ulinzi yanayataka wawepo walinzi watatu katika eneo hilo na kila mmoja alipwe sh.180, 000.

Hafla hiyo fupi ilihudhuriwa na Naibu Waziri (OWM) Kazi, Ajira na Vijana, Bw. Anthony Mavunde, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Binilith Mahenge, Mwenyekiti wa Bodi ya Kituo, Mzee Peter A. Mavunde, Mwakilishi wa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma, Paroko wa Kanisa Kuu Dodoma, Padre Onesmo Wisi, Wajumbe wa Bodi ya Kituo na watendaji kutoka Jiji la Dodoma.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
 S. L. P. 980,
 41193 – DODOMA
JUMATANO, OKTOBA 3, 2018.

No comments:

Post a Comment

Pages