WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali iliamua kutunga Sheria ya Huduma
Ndogo za Fedha ya mwaka 2018 ili kuongeza udhibiti wa sekta ndogo ya
fedha.
“Kwa
muda mrefu sekta ndogo ya fedha haikuwa na udhibiti wa kutosha. Hali
hiyo ilisababisha kuwepo na uendeshaji usio rasmi wa shughuli mbalimbali
za kifedha kama vile, taasisi zinazochukua amana, vikundi vya fedha vya
jamii na wakopeshaji binafsi,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Novemba 16, 2018) bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa 13 wa Bunge. Bunge limeahirishwa hadi Januari 29, mwakani.
Amesema
shughuli hizo ambazo nyingi ziliendeshwa katika utaratibu usio rasmi,
ziliwaletea wananchi athari mbalimbali ikiwemo kupoteza mali zao
zilizowekwa kama dhamana kwenye taasisi hizo.
Amesema
baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu wamekuwa wakitumia mwanya wa
kutokuwepo udhibiti wa kutosha kwenye sekta hiyo ndogo ya fedha
kuendesha vitendo mbalimbali vya kihalifu ikiwemo utakatishaji fedha.
“Kutokana
na sababu hizo, Serikali iliamua kutunga Sheria ya Huduma Ndogo za
Fedha ya mwaka 2018 kwa lengo la kuongeza udhibiti wa sekta hiyo ndogo
ya fedha na kuiwezesha kuchangia ipasavyo katika kuimarisha uchumi wa
nchi yetu na kulinda mali na fedha za wananchi wetu,” amesema.
Serikali
iliwasilisha Muswada wa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha wa mwaka 2018
(The Microfinance Act, 2018) ambao umesomwa kwa hatua zake zote na
kupitishwa na Bunge, ukisubiri kibali cha Mheshimiwa Rais ili uwe sheria
kamili.
Katika hatua nyingine, Waziri
Mkuu amesema hali ya usalama barabarani bado ina changamoto nyingi
licha ya takwimu kuonesha kupungua kwa matukio na vifo vinavyosababishwa
na ajali hizo.
Akitoa
mfano kuhusu matukio ya ajali nchini, Waziri Mkuu amesema katika mwaka
2016 matukio ya ajali za barabarani yalikuwa 9,856 ikilinganishwa na
matukio 5,578 katika mwaka 2017 ambayo ni pungufu kwa matukio 4,278 sawa
na asilimia 43.
Akifafanua
zaidi, amesema katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Oktoba 2018,
matukio ya ajali za barabarani yalikuwa 3,209 ikilinganishwa na matukio
5,578 katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Desemba mwaka jana.
Amesema
Serikali inachukua hatua mbalimbali kukabiliana na matukio ya usalama
barabarani ikiwemo kuendesha operesheni za kuhakikisha sheria zote za
usalama barabarani zinafuatwa kikamilifu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 – DODOMA.
IJUMAA, NOVEMBA 16, 2018.
No comments:
Post a Comment