HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 15, 2018

SERIKALI YAWAPANDISHA MADARAJA WATUMISHI WA UMMA 113,520 WALIOAJIRIWA TANGU MWAKA 2012

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary M. Mwanjelwa (Mb) akijibu swali la Mhe. Joram Hongoli (Mb) Bungeni leo, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora lililohusu upandishwaji wa madaraja kwa watumishi wa umma walioajiriwa mwaka 2012.


 
Serikali imewapandisha madaraja watumishi wa umma 113,520 walioajiriwa mwaka 2012 katika awamu tatu, ambapo ya kwanza walipandishwa vyeo Watumishi 28,049 waliokuwa wameidhinishiwa vyeo kabla ya zoezi la uhakiki wa watumishi hewa na uhakiki wa vyeti kuanzia mwezi Juni, 2016, awamu ya pili ilianza mwezi Novemba, 2017 na ilihusisha watumishi 59,967 ambao taarifa zao zilikuwa kwenye Mfumo Shirikishi wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (HCMIS) kabla ya zuio na awamu ya tatu ilianza mwezi Aprili, 2018 na ilihusisha Watumishi 25,504 ambao barua zao zilikuwa hazijaingizwa kwenye Mfumo. 

Ufafanuzi huo, umetolewa Bungeni leo na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary M. Mwanjelwa (Mb) wakati akijibu swali la Mhe. Joram Hongoli (Mb) kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora lililohusu watumishi wa umma walioajiriwa 2012 kutopandishwa madaraja mpaka hivi sasa. 

Dkt. Mwanjelwa amesema, watumishi walioajiriwa Mwaka 2012 walistahili kupandishwa madaraja kuanzia mwaka 2016/2017 kipindi ambacho Serikali ilikuwa ikifanya zoezi la uhakiki wa watumishi hewa na uhakiki wa vyeti, hivyo mara baada ya kukamilika kwa zoezi hilo Serikali ilianza kuwapandisha watumishi hao kwa awamu hizo tatu kwa kuzingatia vigezo stahiki na
 
 
kuongeza kuwa watumishi wengine ambao wamekidhi vigezo wataendelea kukasimiwa katika bajeti ya mishahara ili waweze kupandishwa vyeo katika mwaka huu wa fedha 2018/2019. 

Aidha, Dkt. Mwanjelwa ameainisha kuwa, watumishi 31,188 walioajiriwa na TAMISEMI mwaka 2012, kati ya hao watumishi 15,320 wamepandishwa vyeo na kubadilishiwa mishahara, na watumishi 3,349 waajiri wao wamewapandisha vyeo lakini majina yao yapo UTUMISHI kwa ajili ya kupitia taarifa zao kabla ya kuwabadilishia mishahara na watumishi 1,064 waliopandishwa vyeo wamebainika kuwa na hoja mbalimbali ambazo waajiri wanapaswa kuzikamilisha na kurejesha majina yao UTUMISHI kwa ajili ya kuwaidhinishia mishahara, watumishi 4,552 hawapo tena katika Utumishi wa Umma na watumishi 6,903 bado hawajapandishwa vyeo ambapo Serikali inatarajia kuwapandishwa vyeo wakati wowote katika mwaka huu wa fedha 2018/19. 

Suala la upandishwaji vyeo kwa Watumishi wa Umma linazingatia vigezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na utendaji kazi mzuri, kukidhi sifa zilizoainishwa katika Miundo ya Maendeleo ya Utumishi, uwepo wa nafasi wazi na bajeti iliyotegwa. Kwa mujibu wa Miundo ya Maendeleo ya Utumishi, mtumishi anapaswa kutumikia cheo kimoja si chini ya miaka mitatu kabla hajafikiriwa kupandishwa cheo.

 Aidha, iwapo mtumishi ameajiriwa kwa mara ya kwanza atapaswa kumaliza mwaka mmoja wa kuthibitishwa kazini kisha ndipo atumikie cheo hicho si chini ya miaka mitatu, hivyo kwa kuzingatia sifa mtumishi anaweza kupandishwa cheo baada ya miaka 3, 4, 5 au hata saba kutegemea na kukidhi vigezo stahiki. 

IMETOLEWA NA: 
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI OFISI YA RAIS (UTUMISHI) TAREHE 15 NOVEMBA, 2018

No comments:

Post a Comment

Pages