HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 20, 2018

DK. MENGI ASHUSHA KOCHA HULL CITY KUIONA SERENGETI BOYS

NA MAKUBURI ALLY



TIMU ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’, imeongezewa nguvu katika benchi lake la ufundi kwa kuongezewa Kocha Andy Mac Millan kutoka Hull City ya Uingereza, kwa ajili ya maandalizi ya kuelekea Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Vijana chini ya miaka hiyo (AFCON-U17), itakayofanyika mwakani hapa nchini.


Upangaji wa ratiba wa fainali hizo, unafanyika leo kwenye Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.


Timu za mataifa ya Nigeria, Angola, Guinea, Cameroon, Morroco, Senegal, Uganda na wenyeji Tanzania ndio watashiriki michuano hiyo mikubwa kwa vijana.


Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mlezi wa Serengeti Boys, Reginald Mengi, alisema kocha huyo atasaidiana na benchi la ufundi kuelekea katika michuano hiyo, ambapo kikosi hicho kinatarajia kushiriki michuano maalum barani Ulaya itakayofanyika nchini Uturuki.


Alisema miezi kadhaa iliyopita aliwahi kueleza kwamba wachezaji wa Serengeti Boys walizaliwa kuwa washindi katika michezo yake itakayocheza na mashindano makubwa inayoshiriki ambako itafanya vizuri hata Kombe la Dunia.


“Hii ni timu yangu naomba ilindwe kwa hali na mali na Watanzania wote, tuliwatuma na wamerudi na ushindi kila waliposhiriki mashindano ya kimataifa, wanastahili zawadi kwa wanayoyatekeleza,” alisema.


Aidha, Mengi alitumia fursa hiyo kumuomba Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe kuwasilisha salam zao kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli kwamba Serengeti Boys hawatomwangusha na wanamuahidi kurejea na Kombe la Dunia, michuano itakayofanyika India.


“Hakuna ambalo haliwezekani chini ya jua, ‘I love you boys’, nitahakikisha vijana hali zao zinakuwa nzuri zaidi katika soka,” alisema.


Naye Waziri Mwakyembe, alisema wamepokea kwa furaha kubwa ushindi wa michuano ya Ukanda wa Kusini mwa Afrika (COSAFA), iliyofanyika Botswana na kuahidi kumfikishia salamu rais kama alivyoeleza mlezi wa timu hiyo.


Alisema Serengeti Boys wameweka rekodi ambayo tangu tupate Uhuru wa nchi hii na kutoa ahadi kwamba vipaji vya vijana hao visipotee hovyo kwa klabu kubwa kujipenyeza na kutaka kuwasajili huku akieleza kwamba wanapoteza muda kwani wachezaji hao haujafikia kufikia hatua ya kusajiliwa.


“Vijana wana bahati ya ajabu sana, wakazane kwa nafasi waliyonayo, wengine wanatuangusha nyinyi hamjatuangusha,” alisema Mwakyembe.


Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, alisema ili kulinda vipaji vya vijana hao ni kuandaa kanzi data (Data base) ya kila mchezaji ili watambue wanapokwenda kwa miaka ijayo.


Karia, alisema anajipanga kubadilisha kanuni kwa klabu zinazowasajili wachezaji hao wawatumie na kama watakosa nafasi watolewe kwa mkopo kwa timu zingine.


Katika hafla hiyo, wachezaji wa Serengeti Boys na benchi la ufundi walikabidhiwa fedha na mlezi, Mzee Mengi, huku akipewa mpira wenye saini za wachezaji na benchi la ufundi.
Mlezi wa timu ya Taifa ya Vijana U17 Serengeti Boys, Dk. Reginald Mengi, akizungumza katika hafla ya kuwapongeza wachezaji wa timu hiyo.

Wachezaji wa timu ya Taifa U17 wakiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe.
Nahodha wa Serengeti Boys, Morris Abraham, akimvisha medali mlezi wa timu hiyo, Dk. Reginald Mengi.

Nahodha wa timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’, Morris Abraham, akimkabidhi kombe la michuano ya COSAFA mlezi wa timu hiyo, Dk. Reginald Mengi, wakati wa hafla ya kuipongeza timu hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam. Kulia ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe na kushoto ni nahodha wa timu hiyo, Moris Abraham.

Mlezi wa timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’, Dk. Reginald Mengi, akinyanyua juu kombe la michuano ya vijana kwa nchi za Kusini mwa Afrika (COSAFA) katika hafla ya kuipongeza iliyofanyika jijini Dar es Salaam. Timu hiyo ilitwaa taji hilo baada ya kuifunga Angola katika fainali. Kulia ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe na kushoto ni nahodha wa timu hiyo, Morris Abraham.


Baadhi ya wachezaji wa timu ya Serengeti Boys wakiwa na medali zao.


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, akiwapa zawadi za fedha wachezaji wa Serengeti Boys baada ya kutwaa ubingwa wa michuano ya vijana kwa nchi za Ukanda wa Kusini mwa Afrika (COSAFA). Fedha hizo zimetolewa na mlezi wa timu hiyo Dk. Reginald Mengi.



Kocha wa makipa wa Serengeti Boys, Peter Manyika, akipokea zawadi yake.

Wachezaji wakipewa zawadi za fulana.

No comments:

Post a Comment

Pages