HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 24, 2018

HALMASHAURI MKOANI TABORA ZAPEWA MWEZI MMOJA KUHAKIKISHA MAJOSHO YANAFANYA KAZI

NA TIGANYA VINCENT

SERIKALI Mkoani Tabora imetoa mwezi mmoja kwa Halmashauri zake zote kuhakikisha majosho mabovu ya kuogeshea ng’ombe yanakarabatiwa na kuanza kufanyakazi ili kuwasaidia wafugaji kuwa na sehemu ya kupeleka mifugo yao kwa ajili ya kuikinga na maradhi.

Kauli hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati akizindua wiki ya uogeshaji ng’ombe kwa Kanda ya Magharibi katika Josho la Itetemia Manisapaa ya Tabora.

Alisema haiwezekani ng’ombe waendelee kufa kwa magonjwa mbalimbali wakati Serikali imenunua dawa aina ya Paranex na kuzisambaza maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kukabiliana na kupe, ndorobo na mbu waenezao ndigana kali ndigana baridi, mkojo mwekundu , homa ya bonde la ufa na maji moyo.

Mwanri alisema ni lazima majosho yote ambayo yamekufa yafufuliwe na yaanze mara moja kutoa huduma kwa wafugaji ili waweze kuwa na uzalishaji wenye tija.

Alisema hatua itasaidia kuongeza ustawi wa wanyama na hatimaye kuongeza uzalishaji na kupunguza vifo vya wanyama vinavyotokana na magonjwa yaenezwayo na kupe na ndorobo.

Naye Afisa Mfawidhi wa Kituo cha Mifugo Kanda ya Magharibi Dkt. Shabani Tozzo alisema jumla ya lita 750 za dawa ya Paranex imepokelewa kwa ajili ya mikoa ya Tabora na Kigoma kwa ajili ya kugawia Halmashauri zote ili zisaidie kukabiliana na kupe na ndorobo.

Alizitaka Halmashauri zote kuhakikisha zinasimamia zoezi la uogeshaji wa mifugo ili kuikinga na vifo vinavyosababishwa na magonjwa yanayoenezwa na kupe na ndorobo.

Aidha Dkt. Tozzo alisema Kanda ya Magharibi (Tabora na Kigoma) ina jumla ya ng’ombe milioni 3.1, mbuzi milioni 1.4, kondoo zaidi ya laki 4, kuku milioni 5.5, nguruwe zaidi ya laki 1 na punda zaidi ya laki 1.

Alisema kanda ya Magharibi ina jumla ya majosho 189 kati ya hayo mazima ni 63 sawa na asilimi 33 ya yote aliongeza kwa Mkoa wa Tabora una jumla ya majosho 111 ambapo mazima ni 18 sawa na asilimia 16.

Akisoma risala ya Chama cha Wafugaji Kikundi cha Ng’ombe Sabho Kata ya Itetemia Makungu Kitula aliomba Serikali kuwaondoa watu waliovamia njia za kupitisha ng’ombe na kuwasababishia usumbufu wakati wa kupeleka mifugo yao mnadani Ipuli.

Aliomba pia Serikali iwasaidie kuwachimbia Bwawa kwa ajili ya kunyeshea mifugo yao ambayo imekuwa ikipata taabu wakati wa ukame.

No comments:

Post a Comment

Pages