HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 07, 2018

Hifadhi ya Ngorongoro yawezesha Mashindano ya Riadha ya Taifa

MASHINDANO ya wazi ya Riadha ya Taifa ya Ngorongoro ‘Ngorongoro National Open Championship 2018’ yanatarajiwa kurindima Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid Kaluta jijini Arusha, Desemba 14 mwaka huu.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam leo, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Wilhelm Gidabuday (pichani), alisema mashindano hayo yamefanikishwa kwa kiasi kikubwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).

Gidabuday, alisema mashindano hayo yatashirikisha wanariadha wa jinsia zote, wanaume na wanawake na ni ruksa kwa mchezaji anayejiona na uwezo kujitokeza kushiriki.

Alisema, mashindano hayo ni muhimu kwa wanariadha kuonyesha viwango vyao, jambo litakalowezesha Kamati ya Ufundi ya Shirikisho kuwa na ‘base’ ya wachezaji walioko kwenye viwango hivi sasa.

“Unajua mwaka uliopita kutoka na kutekeleza kalenda ya RT hatukuwa na mashindano ya Taifa, hivyo tumeona ni lazima mwaka huu vijana wakapata nafasi hii muhimu kuonyesha viwango vyao…Jambo litakalotusaidia pale tutakapokuwa tukifanya uchaguzi wa timu zetu za Taifa kuliko kuwa tukitembelea rekodi za zamani au kutumia mazoea,” alisema Gidabuday na kuwaomba radhi Wanafamilia wote wa Riadha kutokana na kuahirishwa kwa tarehe ya awali.

Alisema kuwa, washindi watakaofanya vizuri zaidi watapata fursa ya kushiriki mashindano mbalimbali ndani na nje ya nchi ikiwamo Japan, kusaka viwango vya kufuzu mashindano ya kimataifa ikiwamo World Championship na Olimpiki.

Awali, RT ilipanga mashindano ya taifa kufanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Novemba 16 kabla ya kuahirishwa ili kupisha yale ya Taifa ya Wanawake yaliyofanyika kwenye uwanja huo Novemba 24 na 25.

Katibu huyo, alisema barua kuitaarifu mikoa kushusiana na mashindano hayo tayari imetumwa na kutoa wito kwa serikali za mikoa kusaidia wanariadha wao wenye viwango kushiriki mashindano hayo.

Alitaja michezo itakayoshindaniwa kuwa ni Mita 100, Relay 100x4, 200, 400, Relay 400x4, 800, 1,500, 5,000 na Mita 10,000, Kuruka Juu, Kuruka Chini, Miruko Mitatu, Kurusha Mkuki, Tufe na Kisahani kwa wanaume na wanawake.

Gidabuday, alisema kutakuwa zawadi kwa washindi, ambako mshindi wa kwanza atapata Medali ya Dhahabu na kitita cha Sh. 150,000 wa pili Medali ya Fedha na Sh. 100,000 huku wa tatu akiondoka na Medali ya Shaba na Sh. 50,000.

Aidha, alitoa wito kwa wadau wengine kuzidi kuiunga mkono Riadha Tanzania kama ambavyo wanavyofanya Ngorongoro.

No comments:

Post a Comment

Pages