HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 25, 2018

RT YAFUNGUKA MAFANIKIO MIAKA MIWILI MADARAKANI

NA SALUM MKANDEMBA

KATIKA kumaliza mwaka wa pili madarakani, Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), limetoa shukrani kwa wadau wa riadha nchini, huku likitambia mafanikio kadhaa ikiwemo uhakika wa kushiriki mashindano makubwa manne duniani yanayokuja.


Katika mujibu wa taarifa ya Katibu Mkuu wa RT, Wilhelm Gidabuday, katika kipindi cha miaka miwili, uongozi wake umemudu kubadili taswira ya shirikisho hilo, ikiwemo kujenga mazingira ya kujitegemea na kustawisha mchezo wa riadha na wanariadha kwa ujumla.


Baadhi ya mafanikio iliyopata katika kipindi hicho ni ofisi za shirikisho, kambi mbili za kudumu Arusha na Mbulu kujiandaa na Olimpiki ya 2020, wadhamini wa kudumu (NCAA na DSTv), wanariadha wa kuaminika (Raia, JKT, Polisi na JWTZ), pamoja na makocha wa kutosha na pia ‘volunteer’ kutoka Japan.


“Novemba 28, 2016 tulipoingia madarakani, tulikuta hakuna ofisi, wafanyakazi hawajalipwa kwa miezi kadhaa, lakini mbaya zaidi tulikuta makato hewa ya NSSF kwa wafanyakazi, mambo yaliyofanywa na uongozi uliopita, lakini kwa sasa tumerekebisha hali hiyo,” ilisema taarifa hiyo.


Kuhusu uhakika wa kushiriki mashindano makubwa mwakani, Gidabuday alisema shirikisho hilo lina uhakika wa wanariadha wa Tanzania kushiriki Mashindano ya Mbio za Nyika za dunia nchini Denmark (Machi 30, 2019) na All African Games, nchini Morocco (Agosti 23 hadi Septemba 3, 2019).


Mashindano mengine Uwanja na Marathon ya Dunia, yatakayofanyika Doha, Qatar (Septemba 28 hadi Oktoba 6,2019), yote hayo yakiwa ni kuelekea Olimpiki ya Majira ya Joto itakayofanyika 2020 mjini Tokyo, Japan ambako Tanzania imepania kurudi na medali.


Gidabuday aliipongeza Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa udhamini uliofanikisha Mashindano ya Wazi ya Riadha yaliyofanyika Arusha Desemba 14 mwaka huu, huku pia akiishukuru Kampuni ya Maltichoice Tanzania (DSTc) kwa juhudi walizozianza tangu 2016.


“Tunaimani NCAA itaendelea kutuwezesha kama tulivyokubaliana kuelekea Olimpiki ya Tokyo, tunawaahidi sisi RT na wanariadha wetu tutangaza maajabu yaliyopo Ngorongoro Crater. Shukurani za kipekee zimwendee Mhifadhi Mkuu kwa zawadi ya kipekee aliyotupatia pale tulipotembelea Crater,” alisema.


Katika suala zima la uwekezaji wa DSTv, Gidabuday alijivunia juhudi zao, zilizomuwezesha Alphonce Felix Simbu kushika nafasi ya tano katika Olimpiki ya Rio de Janeiro Brazil 2016, nafasi ya tano katika 2017 London Olympics na nafasi ya tatu katika Mashindano ya Dunia ya London.


Gidabuday pia amemshukuru Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe kwa uwazi aliojijengea katika kuiongoza wizara hiyo, ambako hasiti kuwaeleza waziwazi viongozi wa vyama vya michezo vyenye mwelekeo wa kumwangusha, huku akipongeza mambo yanapoenda sawa.


“Aidha tunawashukuru sana pia TANAPA kwa udhamini wao wa hivi karibuni, ambapo waliwapatia tiketi za ndege wanariadha wawili walioshiriki Berlin Marathon,” alisema Gidabuday huku akiomba taasisi, mashirika, makampuni na wadau kuendelea kusapoti riadha katika mwaka ujao wa 2019.

No comments:

Post a Comment

Pages