HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 07, 2018

WAZIRI MKUU AMUAGIZA SIMBAKALIA AFUATILIE KIBALI WIZARA YA ARDHI

*Ni cha ujenzi wa kiwanda cha nyuzi Chalinze

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa EPZA, George Simbakalia afuatilie Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuhusu kibali cha ujenzi wa kiwanda cha nyuzi kinachotakiwa kujengwa Chalinze.
Ametoa agizo baada ya Mkuu wa mkoa Pwani, Mhandisi Evarest Ndikilo kumuleza kuwa kuna muwekezaji wa kiwanda cha kutengeneza nyuzi cha H and J cha Chalinze ambacho ujenzi wake umekwama kutokana na mwekezaji kutopewa kibali cha ardhi.
Waziri Mkuu ametoa agzo hilo leo (Ijumaa, Desemba 7, 2018) alipozungumza na wafanyakazi wa kiwanda cha Keda kinachotengeneza marumaru aina ya Twyford kilichopo Chalinze mkoani Pwani akiwa njiani kwenda jijini Dodoma.
Waziri Mkuu amesema ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imedhamiria kuwaunga mkono wawekezaji na kuwafanya wawekeze bila ya urasimu, hivyo amemuagiza kiongozi huyo wa EPZA kuhakikisha kibali kinapatikana.
“Nakuagiza Mkurugenzi ufuatilie kibali hicho na nikifika Dodoma nipate majibu. Hatuwezi kuchelewesha uwekezaji nchini kwa ajili ya urasimu, kila mtendaji ahakikishe anatekeleza majukumu yake ipasavyo.”
Akizungumzia kuhusu uwekezaji katika sekta ya viwanda kikiwemo na kiwanda cha Twyford, Waziri Mkuu amesema uwekezaji huo unafaida kubwa kwani licha ya mapato ya Taifa kuongezeka kupitia kodi pia wananchi wananufaika kwa kupata ajira
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema faida nyingine itokanayo na ujenzi wa viwanda ni pamoja na kutatua changamoto ya masoko ya mazao iliyokuwa ikiwakabili wakulima kwa muda mrefu, hivyo Serikali itaendelea kuhamasisha wawekezaji wengi zaidi.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu ametembelea mradi wa kiwanda cha matunda cha Sayona kilichopo katika kijiji cha Mboga, Chalinze mkoani Pwani na kusema kuwa uwekezaji huo unatija kwa kuwa wakulima wamepata eneo la kuuzia matunda yao.
Waziri Mkuu amesema kwa muda mrefu wakulima wa matunda mbalimbali kama mananasi, maembe katika mkoa wa Pwani na maeneo ya jirani walikuwa hawana soko la uhakika kwa ajili ya kuuzia matunda yao na kusababisha mengi kuharibika.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amewataka wananchi waliopata kazi katika viwanda mbalimbali wawe mabalozi wazuri kwa Taifa na wafanye kazi kwa bidii na uadilifu ili kuviwezesha viwanda hivyo viendelee na uzalishaji na wengine wapate ajira.
Kwa upande wake,Msaidizi wa Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Motisun Group, Aboubakary Mlawa amesema kiwanda cha matunda cha Sayona kimeajiri watumishi 470 kwa sasa huku matarajio ikiwa ni kuajiri watumishi 800.
Amesema licha ya ajira hizo pia mradi huo unawanufaisha wakulima zaidi ya 30,000 kutoka wilayani Bagamoyo kilipo kiwanda pamoja na maeneo mengine yanayolima matunda nchini kwani huuza matunda yao kiwandani hapo.
Akizungumzia kuhusu ujenzi wa mradi huo, Mlawa amesema umegharimu dola za Marekani milioni 55.5, pia kampuni ilitumia sh. milioni 500 kwa ajili ya uwekaji wa umeme mkubwa, uingizaji wa maji pamoja na ujenzi wa barabara kiwandani hapo.
Amesema kiwanda kina uwezo wa kusindika tani 18 za matunda kwa saa kwa line mbili ambazo tayari zimefungwa ila mpango wao ni kuongeza line zingine mbili ambazo zitakuwa na uwezo wa kusindika tani 48 kwa saa, hivyo kiwanda kuweza kusindika tani 66 kwa saa.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, DESEMBA7, 2018.

No comments:

Post a Comment

Pages