NA DENIS MLOWE, IRINGA
CHAMA cha Mapinduzi mkoa wa Iringa, kimemchagua mwadhili wa chuo kikuu cha Ruaha mkoani hapa, Dk. Abel Nyamahanga kuwa mwenyekiti mpya wa chama hicho kuchukua nafasi ya mwenyekiti aliyejiuzulu ambaye kwa sasa ni mkuu wa mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila.
Wajumbe 597 kati ya 631 waliohudhuria wa Mkutano mkuu maalumu wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Iringa wametumia haki yao ya kidemokrasia kwa kufanya uchaguzi wa kumpata Mwenyekiti mpya wa chama hicho chini ya msimamizi wa uchaguzi aliyekuwa waziri mkuu awamu ya nne, Mizengo Pinda.
Mkutano huo maalum uliohudhuriwa na wadau mbalimbali mkoani hapa ulikuwa wa upinzani mkali ambapo kutokana na wajumbe waliozidi akidi ya matakwa ya mkutano wa CCM mkoa kwa mujibu wa maelekezo ya kanuni za uchaguzi wa CCM wajumbe wote ni 631.
Wajumbe hao walitakiwa kuwapigia kura wanachama watatu ambao ni Vitusi Mushi, Amani Mwamwindi na Dk. Abel Nyamahanga ambao majina yao yalirudishwa kutoka kamati kuu ya CCM taifa kwa lengo la kupigiwa kura.
Katika uchaguzi huo uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kichangani, wajumbe walilazimika kurudia uchaguzi kwa awamu ya pili baada ya awamu ya kwanza mshindi kutovuka nusu ya kura zilizopigwa kutokana na upinzani mkali.
Baada ya matokeo kutoka ndipo wa majina mawili ya Amani Mwamwindi na Dk. Abel Nyamahanga yalipigiwa kura kutokana na wajumbe 548 waliobaki baada yaw engine kutoka ukumbini na kuweza kupata mwenyekiti mpya baada ya Vitus Mushi kupata kura chache zaidi ambazo hazikukidhi kanuni za uchaguzi wa CCM.
Hivyo baada ya awamu ya pili ya uchaguzi huo ndipo, Dk Abel Nyamahanga aliibuka kidedea kwa kupata kura 318 kati ya 548 ambapo kura 6 ziliharibika na Aman Mwamwindi kupata kura 224.
Wakizungumza mara baada ya kusaini na kukubali matokeo hayo, Amani Mwamwindi na Vitusi Mushi walilalamikia mchezo mchafu uliokuwepo katika uchaguzi huo hadi kufikia hatua ya msimamizi wa uchaguzi, Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda kumtaka Mushi kuandika malalamiko yake na kuwasilisha ngazi za juu za chama hicho.
Akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi, Mwenyekiti Mpya wa CCM mkoa wa Iringa, Abel Nyamahanga aliwashukuru wapiga kura kwa kumchagua na kuwataka wanaccm kuungana na kuondokana na makundi kwa lengo la kukijenga chama zaidi kuibuka na ushindi katika chaguzi za mitaa.
Nyamahanga amewahakikishia wajumbe na wanachama wa CCM mkoa wa Iringa kuwa atzunguka kata kwa kata kubaini changamoto za wanaccm zinazosababisha kushindwa kuchukua jimbo la Iringa mjini na kuzifanyia kazi na kuanza kwa ushindi wa chaguzi za serikali za mitaa mwaka huu.
Alisema kuwa dhamira ya wanaccm ni moja kuhakikisha serikali na wananchi wanakuwa kitu kimoja na sio kuwagawa kwa misingi ya vyama badala yake ni kupigania chama kinacholeta maendeleo kwa wananchi bila ubaguzi wa vyama na kutaka ushirikiano zaidi kwa wagombea walishika nafasi ya pili na tatu.
Kwa upande wake mlezi wa CCM mkoa wa Iringa ambae pia ni waziri mkuu mstaafu Mizengo Pinda amewataka wanaccm kuhakikisha 2020 Jimbo la Iringa mjini linarudi Ccm pamoja na kata zake kuwataka kuwa kitu kimoja katika kukijenga chama.
Alisema kuwa ataahakikisha anaanza ziara ya kata kwa kata katika mkoa wa Iringa ili kukirudisha chama kwa wanachama kuanzia ngazi za chini na kuahidi kushirikiana na wanachama wote katika kuhakikisha chama kinafata misingi yake.
Aidha alitoa ushauri kwa wagombea ambao hawajaridhika kuandika malalamiko yao kwa ngazi za juu na kuongeza kuwa ni muda muafaka wa wanachama na wajumbe wa ccm kujitathimini ni makosa gani huwa wanafanya wakati wa uchaguzi mpaka jimbo la Iringa kwenda upinzani.
No comments:
Post a Comment