Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC) imetoa wito kwa wapiga kura kwenye uchaguzi mdogo wa kata tatu
utakaofanyika kesho (Jumamosi: 19.01.2019) kujitokeza kwa wingi kupiga kura ili
kuwachagua viongozi wanaowataka wawaongoze kwa kipindi kilichobaki kabla
ya Uchaguzi Mkuu ujao.
Akisoma risala kuhusu
uchaguzi huo Jijini Dar es Salaam leo (Tarehe 18.01.2019) Mwenyekiti wa Tume,
Jaji (Rufaa) Semistocles Kaijage amesisitiza kwamba watakaoruhusiwa kupiga kura
ni wale waliojiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Jaji Kaijage alizitaja kata
zenye uchaguzi kuwa ni pamoja na Kata ya Magomeni katika Halmashauri ya
Manispaa ya Kinondoni Jijini Dar es salaam, Kata ya Mwanyahina katika
Halmashauri ya Wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu na Kata ya Biturana katika
Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo Mkoani Kigoma.
“Kesho Jumamosi tarehe 19
Januari, 2019, ni siku ya Kupiga Kura katika Uchaguzi Mdogo wa Udiwani katika kata
tajwa. Jumla ya Wapiga Kura 26,282
katika Vituo vya Kupigia Kura 69 watahusika na uchaguzi huu mdogo wa Udiwani,”
alisema.
Jaji Kaijage amewaasa
viongozi wa vyama vya siasa, wagombea, wafuasi wao na wananchi kwa ujumla
wajiepushe na vitendo vinavyoweza kusababisha fujo au vurugu wakati wa
uchaguzi.
“Pale panapokuwa na
malalamiko yoyote ya ukiukwaji wa sheria na taratibu za uchaguzi, malalamiko
hayo yawasilishwe kwenye mamlaka inayohusika kwa utaratibu uliowekwa kwa mujibu
wa sheria,” amesema.
Jaji Kaijage amesema kwamba
upigaji kura utafanyika katika vituo vilevile vilivyotumika wakati wa uchaguzi
mkuu wa mwaka 2015 na kuongeza kwamba vituo vitafunguliwa kuanzia saa moja
kamili (1:00) asubuhi na kufungwa saa kumi kamili (10:00) jioni.
“Iwapo wakati wa kufunga
kituo watakuwepo wapiga kura katika mstari, ambao wamefika kabla ya saa kumi
jioni na hawajapiga kura, wataruhusiwa kupiga kura. Mlinzi
wa kituo cha kupigia kura, atasimama nyuma ya Mpiga kura wa mwisho
aliyekuwepo kituoni kabla ya saa 10 jioni. Mtu yeyote hataruhusiwa kujiunga
katika mstari wa wapiga kura baada ya muda huo,” ameelekeza Jaji Kaijage.
Licha ya kusisitiza kwamba
watakaoruhusiwa kupiga kura ni wale tu ambao wamo kwenye Daftari la Kudumu la
Wapiga Kura kwenye Kata husika na wana kadi ya mpiga kura, Jaji Kaijage alisema
kwamba Tume imeruhusu matumizi ya vitambulisho mbadala.
“…..Tume kwa kuzingatia
masharti ya kifungu cha 62(a) cha Sheria
ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, imeruhusu wapiga kura ambao wamepoteza kadi zao za kupigia kura au
zimeharibika au zimechakaa watumie mojawapo ya vitambulisho vifuatavyo; Pasi ya
Kusafiria, Leseni ya Udereva au Kitambulisho cha Uraia kinachotolewa na Mamlaka
ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA),” amesema Jaji Kaijage.
Alifafanua kwamba mpiga
kura ataruhusiwa kutumia vitambulisho hivyo, kwa sharti kwamba jina lake liwemo
katika orodha ya Wapiga Kura katika kituo anachokwenda kupiga kura na lifanane
kwa herufi, maneno na tarakimu na majina yaliyopo katika kitambulisho mbadala.
Jaji Kaijage alisema kwamba
Tume imewaelekeza watendaji wa uchaguzi vituoni wawape kipaumbele wagonjwa,
watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali, wanawake wajawazito au wenye watoto
wachanga na wazee.
Pia ameelekeza kwamba mpiga
Kura mwenye ulemavu wa kutoona, ataruhusiwa kwenda kituoni na mtu atakaemchagua
mwenyewe kwa ajili ya kumsaidia kupiga kura.
“Wapiga kura wanatakiwa
kuondoka vituoni baada ya kupiga kura na
wajiepushe na mikusanyiko au mikutano katika maeneo ya vituo vya kupigia
kura..,” ameagiza.
No comments:
Post a Comment