*Ataka kampuni ya Mzinga Holdings isimamiwe kwa karibu
*Ahimiza tarehe ya mwisho ni Januari 31, mwaka huu
ZIKIWA
zimepita siku 20 tangu akague ujenzi wa mji wa Serikali, Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa amesema ameridhishwa na ujenzi unaoendelea katika eneo
la Mji wa Serikali lililoko Ihumwa.
Hata
hivyo, amesema kampuni ya ujenzi ya Mzinga Holdings inahitaji
kusimamiwa kwa karibu zaidi ili ikamilishe ujenzi wa majengo yake kabla
ya Januari 31, mwaka huu. “Nitakuja kukagua kazi na kupokea funguo za
ofisi siku hiyo,” amesema.
Ametoa kauli hizo leo mchana (Alhamisi, Januari 16, 2019) mara
baada ya kukagua ujenzi wa ofisi za wizara zote pamoja na Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika eneo la Ihumwa lililoko km. 17
kutoka jijini Dodoma.
Waziri
Mkuu ambaye alianza kukagua ujenzi kwenye Ofisi ya Makamu wa Rais,
ametembelea majengo ya wizara zote na kubaini bado kuna changamoto
zinazojitokeza kutokana na utendaji wa mazoea miongoni mwa watumishi wa
Serikali.
Akiwa
katika jengo la Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Waziri Mkuu
alipokea malalamiko kutoka kwa meneja mradi, Bi. Selemina Rwehumbiza
kwamba aliandaa certificate tangu tarehe 13 Januari lakini hadi sasa hajapata malipo. Alipofuatilia, alijibiwa na mshauri mwelekezi kwamba wamepokea certificate hiyo jana jioni (Jumatano, Januari 16, 2019).
“Kama
kazi hii muhimu ya Mheshimiwa Rais, na anayesimamia ni Waziri Mkuu
inacheleweshwa hivi, je akija mwananchi wa kawaida huko ofisini kwenu
atachukua muda gani kupatiwa huduma?,” Waziri Mkuu alimhoji Mshauri
Mwelekezi wa mradi huo kutoka Wakala wa Majengo (TBA), Mhandisi Hilary
Msaki.
“Huu
ni mfano halisi wa malalamiko yanayotoka huko nje kwamba Serikali
haijibu barua za wananchi. Sasa nyaraka kutoka hapa Mtumba inachukua
wiki nzima kwenda mjini, na mtu bado hajajibiwa. Sielewi ni kwa nini
barua iende hadi mjini, wakati wakandarasi wako huku. Kwa nini ninyi
msipokee hizo nyaraka na kuzikimbiza mjini kisha mrudishe majibu hapa site?”, alihoji Waziri Mkuu.
“Kuanzia sasa, kazi zote mpokee ninyi, na ninyi ndiyo mzipeleke huko mjini na kurudi na majibu hapa site kwa wateja wenu, kwani wakandarasi wote wako hapa,” alisisitiza.
Akiwa
katika eneo la Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, Waziri Mkuu alielezwa na Waziri Ummy Mwalimu kwamba wana
changamoto ya kutopatiwa taarifa za maendeleo ya mradi. “Tangu mradi
unaze hatujapewa taarifa hata moja, wakurugenzi wapo wanakuja, lakini
mshauri mwelekezi hatupi ripoti yoyote juu ya huu mradi,” alisema.
Alipohoji
ni kwa nini taarifa hazitolewi, Waziri Mkuu alibaini kuwa hata watu wa
TEMESA pia hawakuwepo kwenye zoezi hilo la ukaguzi. “Niliagiza TBA
wahamie hapa, nao wameweka ofisi yao hapa hapa. Nimeulizia Wakala wa
Ufundi na Umeme (TEMESA) wako wapi, nikaambiwa wako mjini. Ni kwa nini
hawako hapa?” alihoji.
Akizungumza
baada ya kukagua ujenzi wa tangi la maji lenye ujazo wa lita milioni
moja, Waziri Mkuu alisema pamoja na spidi anayoihimiza, bado wakandarasi
wanapaswa kufanya kazi kwa kuzingatia ubora unaotakiwa (quality).
Alisema
kwa ujumla kazi nyingi zimeboreshwa tangu alipokagua mradi huo Desemba
27, mwaka jana. Aliitaka TBA kwa kushirikiana na Kamati ya Kitaifa ya
kuratibu zoezi la Serikali kuhamia Dodoma na Ofisi ya Mkuu wa
Mkoa/Mkurugenzi wa Dodoma wawasimamie wakandarasi na hasa wale wa Mzinga
ili kazi yao ikailike kwa wakati.
“Nimesisitiza katika kila site,
zile kazi ndogondogo zisizohitaji ujuzi au ufundi mkubwa, zigawiwe kwa
vijana ili kuongeza kasi lakini tuzingatie ubora wa kazi,” alisisitiza.
Desemba
27, mwaka jana, Waziri Mkuu alikagua ujenzi wa eneo la Mji wa Serikali
na kubaini kuwa baadhi ya wakandarasi hawaendi na kasi inayotarajiwa na
Serikali. Siku iliyofuata aliitisha kikao cha Mawaziri wote, Makatibu
Wakuu na wakandarasi wao ili waeleze kazi hiyo itakamilishwa lini. Kikao
hicho alikifanyia hukohuko Ihumwa.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 – DODOMA,
ALHAMISI, JANUARI 17, 2019.
No comments:
Post a Comment