WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema
kampuni zote zinazosambaza nguzo za umeme zinatakiwa zilipe ushuru wa
halmashauri wanakotoa nguzo hizo amboa ni asilimia tano ya gharama ya
kila nguzo kama ilivyoelekezwa na Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa.
Ametoa
agizo hilo leo (Jumatatu, Januari 7, 2019) baada ya kupata taarifa
kuhusu kampuni ya New Forest ambayo inamkataba na TANESCO wa kusambaza
nguzo za umeme, kwa muda mrefu kampuni hiyo imekuwa ikikaidi kulipa
ushuru wa asilimia tano ya gharama ya kila nguzo. Ushuru huo umefikia
sh. bilioni 2.9 hali iliyopelekea uongozi wa mkoa kuzuia nguzo hizo
zisitoke.
Wiki
iliyopita akiwa katika ziara ya mkoa Ruvuma, Waziri Mkuu alipokea
malalamiko kuhusu mkoa wa Iringa kuzuia kusambazwa kwa nguzo za umeme
ndipo alipoamua kuwaita Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Happi pamoja na
wakuu wa wilaya, wakurugenzi pamoja na wenyeviti wa halmashauri
wanaotoka katika wilaya zinazozalisha nguzo.
Viongozi wengine waliohudhuria kikao hicho ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye ulemevu, Jenista Mhagama, Waziri
wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, Naibu Waziri Ofisi ya Rais -
TAMISEMI, Josephat Kandege, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu
Kijaji, Naibu Waziri Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhandisi
Stella Manyanya pamoja na maafisa wengine wa Serikali.
Amesema lengo la kikao hicho lilikuwa
kupata ufafanuzuzi kuhusu malalamiko yaliyotolewa dhidi ya uongozi wa
mkoa wa Iringa kuhusu kuzuia usafirishaji wa nguzo za umeme
zinazotomika kwenye miradi ya Kusambaza Nishati ya Umeme Vijiji (REA).
Baada
ya kupata maelezo hayo, Waziri Mkuu amemuagiza mkuu wa mkoa wa Iringa
kuiandikia bili kampuni ya New Forest ili ilipe ushuru huo kuanzia Julai
2018 walipoanza kusambaza nguzo. Asilimia
90 ya nguzo za umeme nchini zinatoka Iringa. Tanzania ina viwanda tisa
vya kutengeneza nguzo na kati ya viwanda hivyo vinane vipo Iringa na
kimoja kipo Tanga.
Kampuni
ilizuiwa kutoa nguzo ndani ya mkoa wa Iringa tangu Novemba 2018 hadi
Januari 2019 huku ikitakiwa kulipa ushuru wa asilimia tano ya gharama ya
kila nguzo ambapo ilikaa ikitaka iendelee kulipa sh. 5,000 kwa kila
nguzo kama walivyokubaliana na TANESCO jambo ambalo ni kinyume cha
sheria.
Hata
hivyo, nguzo za umeme ambazo zilikuwa zimezuiwa kwa muda mrefu katika
maeneo ya uzalishaji hususani mkoani Iringa na kusababisha kukwama kwa
baadhi ya miradi ya usambazaji umeme kwenye baadhi ya mikoa nchini juzi
zimeanza kusambazwa huku taratibu nyingine za malipo zikiendelea.
No comments:
Post a Comment