HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 30, 2019

MADIWANI WA HALMASHAURI YA WILAYA YA TABORA WAPITISHA MAPENDEKEZO YA BAJETI YA BILIONI 35

NA TIGANYA VINCENT, TABORA

HALMASHAURI ya Wilaya ya Tabora –Uyui inatarajia kukusanya jumla ya shilingi bilioni 35 zinatarajiwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2019/20 kutokana na vyanzo vyake vya ndani, ruzuku kutoka Serikali kuu na wadau wa maendeleo.

Taarifa hiyo imetolewa jana na Afisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Tabora Gunah Maziku kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wakati wa kupitia mapendekezo ya bajeti ya mwaka ujao wa fedha.

Alisema katika mapato ya Halmashauri wana lengo la kukusanya shilingi bilioni 2.8 kutoka vyanzo vya ndani.

Gunah alisema wanataraji kupata mapato yanayotokana na ruzuku ya Serikali kuu ya jumla shilingi bilioni 30.8 na wadau wa maendeleo bilioni 1.3

Alisema awa mwaka ujao wa fedha , Halmashauri ya Wilaya ya Uyui mapato ya ndani na vyanzo vingine mbalimbali vitahusu mishahara milioni 115, matumizi ya kawaida bilioni 1.2, miradi ya maendeleo bilioni 1.4, Mfuko wa Afya ya Jamii(CHF) Milioni 153, nguvu za wananchi milioni 350, Mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa(NHIF) milioni 5 na fedha za papo kwa papo milioni 19.6.

Gunah alisema ruzuku ya Serikali kuu itajumuisha mishahara bilioni 23.6, matumizi ya kawaida bilioni 1.6 na miradi ya maendeleo bilioni 5.4

Alisema fedha wanazotarajia kupata fedha za wadau wa maendeleo ambao ni EGPAF milioni 478.5 na Kampuni za ununuzi wa tumbaku milioni 500.

Gunah alivitaja vipaumbele katika bajeti ijayo ni pamoja na kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa kuendelea na ujenzi wa vituo vya kutolewa huduma za afya na ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Uyui , kuboresha elimu ya msingi na sekondari kwa kuendelea na ukamilishaji wa ujenzi wa vyumba vya madarasa na ununuzi wa madawati kwa ajili ya shule hizo na ukamilishaji wa nyumba za walimu.

Aliongeza kuwa kipaumbele kingine kuboresha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kuanzisha stendi za mabasi katika Kata ya Isikizya , Ilolangulu na Kigwa , kuboresha masoko ya bidhaa katika Kata za Tura na Lutende na kuwa na egesho la magari ya mizigo Kata ya Tura.

Gunah alisema mkakati wa kuimarisha mapato kwa kununua mashine 90 za kielektroniki kwa ajili ya ukusanyaji wa kodi, ushuru na tozo ili kudhibiti upotevu wa mapato.

Aliongeza kuwa kuanzisha miradi ya maendeleo ya kimkakati yenye lengo la kuongeza mapato ya ndani ikiwemo ujenzi wa stendi za mabasi, ujenzi wa bwawa na skimu ya umwagiliaji kilimo cha mpunga katika Kata ya Loya na ujenzi wa kiwanda cha chakula cha mifugo katika Kata ya Isikizya.

No comments:

Post a Comment

Pages