HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 14, 2019

DKT. MWANJELWA AAGIZA KUPEWA MCHANGANUO WA MATUMIZI YA SHILINGI MILIONI 101 ZILIZOTOLEWA NA TASAF KUJENGA UZIO WA SHULE MAALUM

  Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akizungumza na wanafunzi na walimu wa Shule Maalum ya Msingi Pongwe pamoja na wakazi wa mtaa wa Pongwe Kaskazini, jijini Tanga, alipotembelea shule hiyo kwa lengo la kukagua, kujionea na kujiridhisha na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa uzio katika Shule hiyo, ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi mkoani humo yenye lengo la kukagua miradi ya TASAF na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma.
 
Katibu Tawala Mkoa wa Tanga, Bi. Zena Said akimkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) kuzungumza na wanafunzi na walimu wa Shule Maalum ya Msingi Pongwe pamoja na wakazi wa mtaa wa Pongwe Kaskazini, jijini Tanga, katika siku ya kwanza ya ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo mkoani humo yenye lengo la kukagua miradi ya TASAF na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma.
  Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akimuagiza Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Bw. Daudi Mayeji (hayupo pichani) kuwasilisha mchanganuo wa matumizi ya fedha zilizotolewa na TASAF kwa lengo la kujenga uzio ili kuimarisha usalama wa wanafunzi wa jamii ya albino katika Shule Maalum ya Msingi Pongwe jijini Tanga.
 Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akishiriki kuimba wimbo na wanafunzi wenye mahitaji maalum  wa Shule Maalum ya Msingi Pongwe ya jijini Tanga, alipotembelea shule hiyo kwa lengo la kukagua, kujionea na kujiridhisha na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa uzio katika Shule hiyo wenye lengo la kuimarisha ulinzi na usalama wa wanafunzi wa jamii ya albino katika shule hiyo.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akifurahia jambo na wanafunzi wenye mahitaji maalum wa Shule Maalum ya Msingi Pongwe ya jijini Tanga, alipotembelea shule hiyo kwa lengo la kukagua, kujionea na kujiridhisha na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa uzio katika Shule hiyo wenye lengo la kuimarisha ulinzi na usalama wa wanafunzi wa jamii ya albino katika shule hiyo. 


TANGA, TANZANIA


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb), amemtaka Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Bw. Daudi Mayeji kuwasilisha mchanganuo wa shilingi 101, 089,736.65/= zilizotolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kujenga uzio wa Shule Maalum ya Msingi Pongwe kwa lengo la kuimarisha ulinzi na usalama wa wanafunzi wa jamii ya albino katika shule hiyo.
Agizo hilo amelitoa jijini Tanga, alipotembelea mradi wa ujenzi wa uzio katika shule hiyo maalum ili kujionea na kujiridhisha na utekelezaji wa mradi huo, ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi mkoani humo yenye lengo la kukagua miradi ya TASAF na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma mkoani Tanga.
Mhe. Dkt. Mwanjelwa amefafanua kuwa, licha ya kuridhika na kazi nzuri iliyofanywa na Mkurugenzi huyo pamoja na wasaidizi wake ya ujenzi wenye viwango, lakini anataka maelezo ya kina ya matumizi ya fedha hizo baada ya kuangalia uzio uliojengwa na kiwango cha fedha kilichotolewa na  TASAF  ambapo  ameelezwa kwamba gharama za uzio huo ni shilingi milioni 75 hivyo, anataka kujua kiasi kilichobakia kimetumikaje.
Mhe. Dkt. Mwanjelwa ameongeza kuwa fedha iliyotolewa na TASAF imefanya kazi nzuri na kusisitiza kuwa, fedha iliyotolewa kutekeleza mradi wa ujenzi wa uzio huo ni lazima kazi yake iwe ya kiuhalisia kulingana na fedha iliyotolewa na sio vinginevyo.
Awali, akiwasilisha taarifa ya ujenzi wa uzio huo, Kaimu Mtendaji, Mtaa wa Pongwe, Bi. Dorah Senkondo amesema, ujenzi wa uzio wa mita 738 katika Shule Maalum ya Msingi Pongwe utaimarisha ulinzi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum ambao ni walemavu wa ngozi kutokana na changamoto ya kiusalama iliyopo kwa jamii ya albino.
Bi.  Senkondo  ameainisha kuwa, serikali kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini, imetoa kiasi cha shilingi 101, 089,736.65/= ikiwa ni fedha za awamu ya kwanza ili kutekeleza ujenzi wa mradi huo, ambapo jumla ya mita 496 zimejengwa hadi hivi sasa, hivyo kubakiza ujenzi wa uzio wa mita 242  utakaokamilika kupitia fedha za awamu ya pili zitakazotolewa.
Ujenzi wa uzio huo unahusisha mchango wa jamii na usimamizi kutoka katika Halmashauri ya jiji la Tanga ili kuweza kufikia lengo la kuimarisha ulinzi na usalama kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum wa Shule ya Msingi Pongwe iliyopo mtaa wa Pongwe Kaskazini jijini Tanga.


IMETOLEWA NA;
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
OFISI YA RAIS (UTUMISHI)
 TAREHE 14 FEBRUARI, 2019
 

No comments:

Post a Comment

Pages