HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 14, 2019

TMA yatabiri mvua nyingi masika

NA MWANDISHI WETU
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetabiri kuwepo kwa mvua za nyingi za masika zitakazoanza mwisho mwa Februari,2019 na kumalizika mwanzoni mwa Mei.
Hata hivyo vitakuwepo vipindi vya mvua haba maeneo kadhaa ya Kaskazini mwa mikoa ya Kigoma na Morogoro.
Akizungumzia mwelekeo wa mvua za masika zinazotarajiwa kunyesha kati ya Machi, Aprili na Mei mwaka huu, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agnes Kijazi, alisema mvua za masika mwaka huu zitawahi  kunyesha na kuwahi kumalizika.
Mbele ya waandishi wa habari waliofika ofisini kwake jana, Dk. Kijazi alisema kutokana na hali hiyo wananchi katika sekta mbalimbali wanatakiwa kuchukua tahadhari na kufuatilia utabiri wa siku 10 ili kutekeleza majukumu kulingana na hali ya hewa.
Alisema kwa kutumia mifumo mbalimbali ya hali ya hewa, kabla ya changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi na hali ya hewa mifumo haibadiliki tofauti na sasa ambapo hubadilika na kusababisha tabiri za mamlaka hiyo pia kubadilika.
Alisema mvua za wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka hata hivyo baadhi ya maeneo ya nyanda za Juu Kaskazini Mashariki yanatarajiwa kupata mvua za wastani na juu ya wastani.
Alisema katika maeneo ya nyanda za Juu Maskazini Mashariki, Pwani ya Kaskazini na Visiwa vya Unguja na Pemba, Ukanda wa Ziwa Viktoria na Kaskazini mwa Kigoma sehemu kubwa wanatarajia kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.
Dk. Kijazi alieleza kuwa katika baadhi ya maeneo ya nyanda za Juu Kaskazini–Mashariki hasa mikoa ya Arusha na Kilimanjaro, kuna uwezekano wa kupata mvua za juu ya wastani.
Alisema ukanda wa Pwani ya Kaskazini, mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Visiwa vya Unguja na Pemba na Kaskazini mwa Morogoro mvua zitaanza mwishoni mwa mwezi huu na kuwa za wastani hadi juu ya wastani huku kaskazini mwa Morogoro kukiwa na mvua haba.
Alisema katika nyanda za juu Kaskazini Mashariki katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara mvua zinatarajia kuanza mwishoni mwa Februari na kuwa juu ya wastani hadi wastani.
Kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa Viktoria hasa Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu na Shinyanga mvua zinatarajia kuanza mwisho wa mwezi huu na Kagera na kusambaa maeneo mengine kwa kiwango cha wastani au juu ya wastani.
Kuhusu mvua za msimu zilizoanza Novemba mwaka jana kwa maeneo yanayopata mvua mara moja kwa mwaka, mkurugenzi huyo alisema mvua zinatarajia kuendelea mpaka mwishoni mwa Aprili mwaka huu.
Dk. Kijazi alisema mvua chini ya wastani zinatarajiwa katika maeneo machache ya kanda ya Kusini na mikoa ya Dodoma na Singida huku akisisitiza kwamba msimu huo vipindi vya ukame vitajitokeza hivyo maofisa ugani wanatakiwa kuwaelimisha wakulima kupanda mazao yanayovumilia ukame na wafugaji kutunza malisho.
Akitoa tathmini ya utabiri wa hali ya hewa kwa msimu wa mvua za vuli uliopita, Meneja Kituo Kikuu cha Utabiri, Samwel Mbuya, alisema katika utabiri wa vuli, mvua zilianza kwa wakati ukanda wa Ziwa Viktoria na kunyesha kama ilivyotarajiwa.
Alisema licha ya kuchelewa, mvua na sehemu nyingine mtawanyiko wa mvua haukuwa wa kurithisha hivyo utabiri kuwa sahihi kwa asilimia 80.

No comments:

Post a Comment

Pages