HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 26, 2019

MAGDALENA AIBEBA NGOME MITA 1500 BAMMATA

Magdalena aipa dhahabu ya kwanza Ngome Riadha BAMMATA

NA TULLO CHAMBO



MASHINDANO ya Majeshi ya Ulinzi na Usalama (BAMMATA), yamezidi kushika kasi kwenye viwanja tofauti jijini Dar es Salaam, ambako kwa jana mchezo wa Riadha ulianza kurindima kwenye Uwanja wa Taifa huku timu ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Ngome, ikianza kwa kutwaa medali ya dhahabu mita 1,500.

Alikuwa ni Mshindi wa pili wa mashindano ya Taifa ya Mbio za Nyika mwaka huu ‘Ngorongoro National Cross Country 2019’ yaliyofanyika Februari 16 mjini Moshi, Kilimanjaro, Private Magdalena Shauri, ndiye aliyeipa Ngome medali ya kwanza ya dhahabu mita 1,500 baada ya kutumia dakika 4:38.60 huku akipata upinzani kutoka kwa mwenzake Private Cecilia Ginoka pia wa Ngome aliyetumia dakika 4:38.60 na kutwaa medali ya fedha.

Wanariadha wa Jeshi la Kujenga (JKT), walifuatia baada ya Private Angelina Tsere kutwaa medali ya shaba akishika nafasi ya tatu akitumia dakika 4:38.60.

Nafasi ya nne ilikwenda kwa SG Amina Mgoo wa JKT aliyetumia dakika 4:44.63 huku nafasi ya tano pia ikienda kwa SG Grace Charast aliyetumia dakika 4:45.63 wakati Mariya Benedito wa Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), akishika nafasi ya sita akitumia dakika 5:38.78.

Akizungumzia siri ya mafanikio yake, Magdalena alisema ni uzoefu, kujituma na nidhamu ya mazoezi ambayo waliandaliwa vema chini ya Makocha wao Anthony Mwingereza akisaidiwa na Philipo Kandau chini ya Matron wao, Mwanariadha mahiri wa zamani wa Taifa, Restituta Joseph.

Mchezo mwingine wa fainali jana ulikuwa ni Kutupa Tufe wanaume na wanawake.

Michezo mingine iliyochezwa jana hatua ya mchuano ni Mita 100 wanawake na wanaume na Mita 200.

Leo Riadha itaendelea kutimua vumbi kwenye Uwanja wa Taifa, ambako kutakuwa na fainali Kutupa Kisahani Wanaume na Wanawake, Mita 100 Wanaume na Wanawake.

Ila uhondo unatarajiwa kuwa katika fainali ya Mita 1,500 Wanaume, ambayo kama ilivyokuwa kwa Wanawake jana, ambako wanariadha wenye majina kama Faraja Damas, Mohamed Mbua wa Ngome, Elibariki Buko wa JKT, Bazil John, Bazil Sulle, Emmanuel Gadie wa Polisi, Enock Benjamin na Hiti Emmanuel wa Magereza wataonyeshana kazi.

No comments:

Post a Comment

Pages