Na
Benny Mwaipaja, WFM, Kibaha
Serikali imetoa zaidi ya
sh. bilioni 42 kwa ajili ya kukarabati miundombinu ya Sekondari 42 kati
ya shule 88 kongwe zilizopo nchini kote ikiwemo shule ya Sekondari Ruvu iliyoko
Wilayani Kibaha Mkoani Pwani.
Akizungumza mara baada ya kukagua ukarabati wa shule hiyo,
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango. Dkt. Ashatu Kijaji, amesema kuwa lengo la
Serikali ni kuhakikisha kuwa shule zote Kongwe ambazo zinahistoria kubwa ya
kutoa viongozi wengi na wataalam mbalimbali nchini, zinakuwa na hadhi na kuwa
kimbilio la wananchi.
Ametoa wito kwa uongozi wa
shule hiyo ya Sekondari ya Wasichana Ruvu, kuhakikisha kuwa elimu bora inatolewa
kwa wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo ili thamani ya uwekezaji mkubwa wa
Serikali unaofikia zaidi ya shilingi milioni 990 uweze kuonekana
"Dhamira yetu ni
kuona watoto wetu wanasoma kwenye mazingira sahihi na ufaulu wao unaongeeaka
kwa sababu tunawaandaa wataalam wa kesho wa Taifa letu" Aliosisitiza Dkt.
Kijaji
Alisema amejionea
ukarabati uliofanyika shuleni hapo ambapo pamoja na shilingi milioni 992
kutumika katika ukarabati huo, bado nyumba 6 za walimu hazijakarabatiwa pamoja
na kutonunuliwa kwa samani za shule vikiwemo vitanda na kuahidi kuifanyia kazi
changamoto hiyo wakati wa huu wa mchakato wa bajeti mpya
Kwa upande wao, Mbunge wa
Kibaha Vijijini, Hamoud Juma na Mkuu wa Shule hiyo, Juliana Chimazi, wameishukuru
Serikali kwa kutoa fedha kwa ajili ya kuboresha shule hiyo na kuomba wapatiwe
fedha kwa ajili ya kununulia samani hasa vitanda kwa ajili ya wanafunzi ili
kwenda sambamba na uboreshaji mkubwa wa majengo uliofanyika shuleni hapo.
Mkuu wa shule hiyo Mwl.
Juliana Chimazi alimweleza Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji
kwamba shule hiyo inahitaji vitanda vipya kwa kuwa vilivyopo vimedumu zaidi ya
miaka 50 pamoja na kuomba fedha kwa ajili ya kukamilisha ukarabati wa nyumba
sita za walimu.
Miongoni mwa miundombinu
iliyoboreshwa katika shule hiyo ya Sekondari ya washichana Ruvu ni pamoja na mifumo
ya maji taka, madarasa, vyoo, mabweni, nyumba za walimu na Ofisi.
Naibu Waziri Dkt. Kijaji
anaendelea na ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali iliyopewa fedha na
Serikali ikiwemo ya kimkakati inayolenga kuziwezesha Mamlaka za Serikali za
Mitaa nchini kujitekemea kwa mapato.
No comments:
Post a Comment