HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 23, 2019

Msama afariji vituo sita vya watoto yatima Dar

 Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotions, Alex Msama, akimkabidhi sehemu ya msaada wa vitu mbalimbali, mtoto Kwaya Emmanuel (8), wa Kituo cha Yatima cha Watoto Wetu Tanzania. Hafla hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam. (Picha na Francis Dande).

NA DEODATUS MKUCHU

WARATIBU wa Tamasha la Pasaka, kampuni ya Msama Promotions Ltd ya jijini Dar es Salaam, leo Februari 23 imetoa msaada kwa vituo sita vya kulea watoto yatima na waliopo katika mazingira magumu katika mkoa wa Dar es Salaam.

Misaada hiyo ambayo imekuwa faraja kwa vituo hivyo, ni utekelezaji wa moja ya maudhui ya Tamasha hilo ambalo limekuwa linafanyika kila mwaka tangu mwaka 2000.

Akikabidhi misaada hiyo kwa viongozi wa vituo hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha hilo, Alex Msama alisema kuwa wameendelea kufanya hivyo kutimiza wajibu wa kusaidia makundi maalumu katika jamii.

“Tunetoa msaada huu kutoka katika mfuko wa Tamasha la Pasaka, sio kusema, tuna uwezo mkubwa sana, bali kutambua umhimu wa kila mmoja mwenye nacho hata kama ni kidogo, kusaidia wenye uhitaji,” alisema.

Msama alisema yeye na Kamati yake wanajisikia faraja kubwa kuona wanatoa kidogo walichojaaliwa kwa vituo hivyo vyenye jukumu zito la kulea watoto kwa kuwapatia mahitaji ya msingi ikiwamo chakula.

Vikundi vilivyopatiwa msaada huo wa vitu mbalimbali, ni pamoja na Mwandaliwa cha Boko, Sifa (Bunju), Maunga (Kinondoni), Zaidia cha Sinza, Watoto wetu Tanzania na Honoratha.

Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na mchele, unga, soda, sabuni, maji, mafuta ya kupikia, juis, Sukari na vinginevyo ambavyo vimepeleka shangwe kwa watoto, walezi na wamiliki wa vituo hivyo.

Msama alisema msaada huo wa vitu mbalimbali, ni katika kutimiza moja ya maudhui ya Tamasha la Pasaka la kuyajali na kuyafariji makundi maalumu wakiwamo yatima, walemavu na wajane.

Alisema wameona watoe zawadi hiyo sasa kwa kutambua jukumu zito linalobebwa na wamiliki wa vituo hivyo hasa katika kipindi hiki kigume cha hali ya fedha kama ilivyo kwa watu wengi kote nchini.

“Tumetoa msaada huu kwa kutambua wajibu wetu kama sehemu ya jamii kusaidia makundi kama haya, hivyo tumetoa misaada hii kipindi hiki cha maandalizi ya Tamasha la Pasaka,” alisema Msama.

Alisema suala la kutoa msaada kwa makundi hayo maalumu katika jamii, ni sehemu ya maudhui ya tukio hilo tangu kuanzishwa kwake iwe kabla ama baada ya kufanyika.

Msama ametoa wito kwa watu wengine wenye uwezo hata kama ni mdogo na mapenzi mema na watoto, wajitokeze kuwasadia kama kutimiza wajibu wao wa kurejesha shukrani kwa Mungu.

Kuhusu Tamasha lenyewe, Msama alisema maandalizi yanakwenda vizuri ambapo baada ya kuzinduliwa jijini Dar es Salaam Aprili 21, moto wake utasambaa katika mikoa ipatayo 10 ya Tanzania Bara.

Mbali ya tukio hilo kuwa faraja kwa makundi maalumu, malengo mengineyo ni pamoja na kueneza ujumbe wa Neno la Mungu, kukuza muziki wa injili na kuhimiza amani na upendo katika Taifa.

No comments:

Post a Comment

Pages