Mwekezaji wa Simba, Mohamed Dewji 'MO' akishuhudia pambano la Simba na Al Ahly kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. (Picha na Said Powa).
Mashabiki wa Simba wakishangilia.
Kikosi cha Al Ahly.
Meddie Kagere akimiliki mpira huku akizongwa na beki wa Al Ahly.
Meddie Kagere akimiliki mpira huku akizongwa na beki wa Al Ahly.
Mshambuliaji wa Simba, John Bocco, akishangilia bao lililofungwa na Meddie Kagere katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly Misri. Simba ilishinda 1-0.
Wachezaji wa Simba, Meddie Kagere (kushoto), Cletus Chama (katikati), na John Bocco (kulia), wakishangilia bao la ushindi dhidi ya Al Ahly lililofungwa na Kagere katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF CL), kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mashabiki wa Simba wakishangilia.
Na John Marwa, Dar es Salaam, Tanzania
HAWAAMINI! Yeyote hawezi kutoka uwanja wa Taifa ‘kwa Mchina’, usemi huo umedhihirika jana baada ya wawakilishi pekee wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa barani Afrika(CAF-CL), Simba SC leo Februari 12, 2019 walipomtuliza bingwa wa Kihistoria, National Al Ahly ya Misri.
Simba walishuka Dimba la Taifa jana wakiwa majeruhi baada ya kutoka kupokea kipigo cha mabao 5-0 kutoka kwa Waarabu hao huko Alexandria, Misri, hivyo jana kulipa kisasi ilikuwa ni lazima.
Ikicheza kwa nidhamu ya hali ya juu, Simba iliweza kuwapa raha Watanzania baada ya kuwalaza kwa bao 1-0 Waarabu hao kwenye Uwanja wa Taifa na kuwaacha wakibaki na butwaa na kutoamini kile kilichotokea.
Kwa ushindi huo, Simba imefufua matumaini ya kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo mikubwa barani Afrika ngazi ya klabu.
Idadi kubwa ya mashabiki walikuwa na wasiwasi kwamba Simba inaweza kupoteza mchezo wa jana kwa kukubali kichapo cha mabao kama iliyopigwa kwenye mechi mbili za michuano hiyo.
Hata watani zao, Yanga waliamini kwamba, Simba atapokea kichapo kingine kutoka kwa Al Ahly, hali ambayo haikuwa kama walivyodhani.
Simba waliingia uwanjani kwa kujiamini na kujituma zaidi, hali ambayo iliamsha ari ya aina yake kwa wapenzi na mashabiki wa timu hiyo.
Meddie Kagere ndiye shujaa aliyepeleka kilio nchini Misri na kufufua matumaini ya kwenda robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kupachika bao hilo.
Kagere raia wa Rwanda aliyetua Msimbazi akitokea Gor Mahia ya Kenya, alifunga bao hilo dakika ya 65 kwa shuti la mguu wa kulia akimalizia pasi ya kichwa ya Nahodha John Bocco aliyepokea krosi ya beki Zana Coulibaly kutoka Burkina Faso.
Kwa ushindi huo, Simba SC inafikisha pointi sita baada ya kucheza mechi nne ikipanda kwa nafasi moja hadi ya pili, nyuma ya Al Ahly wenye pointi saba na kuishusha kwa muda AS Vita ya DRC yenye pointi nne na JS Saoura ya Algeria yenye pointi mbili.
Simba jana iliingia uwanjani ikitoka kujeruhiwa kwa kipigo cha mabao 5-0, mchezo uliochezwa Februari 2 mjini Alexandria.
Kabla ya kipigo hicho, mwishoni mwa Januari, Simba ilitoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ambako pia ilikubali kichapo cha mabao 5-0 kutoka kwa AS Vita.
Simba ilianza hatua hiyo ya makundi kwa kishindo ikiwachapa JS Saoura ya Algeria kwa mabao 3-0 kwenye Dimba la Taifa jijini Dar es Salaam, kabla ya mambo kuharibika huko Congo DR na Misri.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania bara (TPL), sasa watahamishia makali yao kwenye Ligi wakimenyana na watani wao wa jadi, Yanga SC Jumamosi kabla ya kusafiri kuwafuata JS Saoura Machi 9 kabla ya kurejea nyumbani kumalizia na AS Vita Machi 16.
No comments:
Post a Comment