Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb) akizungumza na wanufaika
wa TASAF wa kijiji cha Mkwanyule wilayani Kilwa katika mkutano uliofanyika
kwenye viwanja vya shule ya msingi Mkwanyule wilayani humo. Kulia kwake ni Mkuu
wa Wilaya ya Kilwa Mhe. Christopher Ngubiagai.
Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mhe. Christopher Ngubiagai akimkaribisha Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb), kuzungumza na wanufaika wa TASAF wa
kijiji cha Mkwanyule wilayani Kilwa (hawapo pichani) katika mkutano uliofanyika
kwenye viwanja vya shule ya msingi Mkwanyule wilayani humo.
Wakazi wa kijiji cha Mkwanyule wilayani Kilwa wakimsikiliza Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt
(Mst) George Mkuchika (Mb) (hayupo pichani) katika mkutano wa Waziri
huyo na wanufaika wa TASAF uliofanyika katika viwanja vya shule ya msingi
Mkwanyule wilayani Kilwa.
Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kusini, Mhe. Selemani Bungara akiishukuru
serikali kwa kuufikisha Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wilayani kwake wakati
wa mkutano kati ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb) na wanufaika
wa TASAF uliofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Mkwanyule wilayani
humo.
Mmoja wa wanufaika wa TASAF mkazi wa kijiji cha Mkwanyule Bi.
Mwanahamisi Ally Ukwenda akishuhudia namna alivyonufaika na TASAF wakati wa
mkutano kati ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb) na wanufaika wa
TASAF uliofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Mkwanyule wilayani Kilwa.
Kushoto kwake ni mnufaika mwenzie Bi. Atili Masoud Swalehe.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb) (kulia) akikagua mradi wa
mbuzi unaomilikiwa na Bw. Hassan Charahani (kushoto) mara baada ya kumaliza
mkutano kati yake na wanufaika wa TASAF uliofanyika katika viwanja vya shule ya
msingi Mkwanyule wilayani Kilwa. (Picha na Ofisi ya Rais-Utumishi)
NA MWANDISHI MAALUM, KILWA
Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb) amepongeza
jitihada za Wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) wa kijiji cha
Mkwanyule wilayani Kilwa za kujikwamua kiuchumi kwa kutumia vizuri fedha za
TASAF.
Pongezi hizo amezitoa
wakati wa mkutano kati yake na
wakazi wa Kijiji cha
Mkwanyule wilayani Kilwa uliofanyika
kwenye viwanja vya shule ya msingi Mkwanyule wilayani humo.
Mhe. Mkuchika ametoa
pongezi hasa kwa kinamama kwa kutumia vizuri fedha hizo katika kuzalisha miradi
ya maendeleo na amefurahishwa na ushuhuda wa akina mama ambao mwanzoni walitumia
vibaya fedha hizo lakini baadae wakawekeza katika miradi ya maendeleo.
Mhe. Mkuchika ametoa
ufafanuzi kuwa lengo la kuanzishwa kwa TASAF ni kupambana na umaskini ili
kuboresha hali duni za Watanzani na kuagiza wanufaika wa TASAF kutofanyia mzaha
fedha wanazozipata.
Aidha, Mhe. Mkuchika amepongeza
wasimamizi wa TASAF katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa akiwemo Mkuu wa
Wilaya, Mkurugenzi na Mratibu wa TASAF wa halmashauri hiyo kwa kusimamia vizuri
utekelezaji wa miradi ya TASAF.
Akitoa ushuhuda katika
mkutano huo, mmoja wa wanufaika wa TASAF mkazi wa kijiji cha Mkwanyule, Bi. Mwanahamisi
Ukwenda, ameishukuru serikali kwa kuianzisha TASAF kwani imemuwezesha kufanya
shughuli za ufugaji wa kuku na mbuzi na kupata fedha ambazo zinamsaidia kwa
mahitaji maalumu mara anapouza mifugo hiyo.
Aidha, Bi. Mwanahamisi
amekiri kutotumia vizuri fedha za TASAF alizozipata katika awamu ya kwanza na
ya pili na kuahidi kuendelea kuzitumia vizuri fedha hizo kwa sasa.
Mnufaika mwingine, Bw.Hassan Charahani ameushukuru mradi wa TASAF kwa
kumkwamua kwenye umaskini kwani hapo awali alikuwa akila mlo mmoja kwa siku na
hakuweza kusomesha watoto lakini TASAF imebadili maisha yake.
Kwa upande wake Mbunge wa Kilwa
Kusini, Mhe. Selemani Bungara ameishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa kuwezesha wakazi wa kijiji cha Mkwanyule kuwa na miradi ya ufugaji
kuku, mbuzi na kujenga bwawa la maji na pia ameipongeza serikali kwa kutokua na
ubaguzi katika kuleta maendeleo nchini kwa kuwa Mkwanyule inaongozwa na
viongozi wa chama cha CUF.
Mhe. Mkuchika anaendelea na ziara
ya kikazi mkoani Lindi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa
umma pamoja na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani humo.
No comments:
Post a Comment