HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 03, 2019

WAIMBAJI 5 WA KIMATAIFA KUBEBA TAMASHA LA PASAKA

 Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotions, Alex Msama, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, kuhusu maandalizi ya Tamasha la Pasaka litakaloanza kutimua vumbi Aprili 21, 2019. (Picha na Francis Dande).
 Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotions, Alex Msama, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, kuhusu waimbaji wa nyimbo za injili watakaoshiriki tamasha la Pasaka wawe wamesajiliwa na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata).




NA MWANDISHI WETU

MAANDALIZI ya Tamasha la Pasaka litakalozinduliwa Aprili 21, jijini Dar es Salaam, yamezidi kushika kasi, baada ya kukamilika kwa mazungumzo na waimbaji maarufu watano kutoka nje.

Hayo yalibainishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha hilo, Alex Msama ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Msama Promotions Ltd inayoratibu tukio hilo la kimataifa.

Alisema, ingawa hatuwezi kuwataja kwa sasa kwa sababu wakati wa kufanya hivyo bado, tumeshazungumza na waimbaji maarufu wa Afrika Kusini, Nigeria, Zambia, Rwanda na Uingereza.

“Hadi sasa tumekamilisha mazungumzo na waimbaji kutoka nchi tano. Tumeshazungumza na waimbaji maarufu wa Afrika Kusini, Nigeria, Zambia, Rwanda na Uingereza,” alisema Msama.

Alisema ya kuwa, kamati yake imepanga kuwa na waimbaji watano wa kutoka nje na wengine sita ni waimbaji mahiri wa hapa nchini.

Msama alisema wamepanga kuwa na waimbaji wachache katika tukio hilo ili waweze kupata bafasi ya kutosha katika kuonyesha uwezo na umahiri wao katika huduma hiyo.

Kwa upande wa waimbaji wa ndani, Msama amesema kigezo kimojawapo cha mwimbaji kupata nafasi ya kushiriki Tamasha hilo, ni awe amesajiliwa Baraza la Sanaa Tanzania (Basata).

Mbali ya kusajiliwa, pia mwimbaji husuka anapaswa awe ni mwanachama hai, kwa maana ya kulipa michango yake kwa mujibu wa taratibu, vinginevyo atakosa sifa ya kushiriki.

“Nitoe wito kwa waimbaji wa hapa nchini, kigezo cha kwanza kuteuliwa kushiriki Tamasha la Pasaka, ni awe amesajiliwa Basata na uwe mlipaji mzuri wa ada za uanachama,” alisema.

Kwa upande wa Tamasha lenyewe, Msama alisema baada ya kutikisa jijini Dar es Salaam, itakuwa zamu ya kwenda mikoani, wakianzia Dodoma, Singida, Mwanza, Simiyu na kwingineko.

Kuhusu malengo, Msama alisema mbali ya kufikisha Neno la Mungu kupotia uimbaji, litatumika pia kuhimiza hali ya amani, umoja na mshikamano uliopo katika taifa.

Alisema ni muhimu kuenzi hali ya amani kwa kuzingatia, ndio msingi wa kila kitu kwa sababu bila amani, hakuna jambo la maendeleo linaloweza kupangwa na kufanikiwa ipasavyo.

No comments:

Post a Comment

Pages