Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotions, Alex Msama, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, kuhusu maandalizi ya tamasha la Pasaka. Kushoto ni Mjumbe wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Saleh Mohamed. (Picha na Francis Dande).
NA MWANDISHI
WETU
WAKATI
maandalizi ya Tamasha la Pasaka yakizidi kushika kasi, shauku kubwa ya wadau wa
muziki wa injili, ni kujua vichwa gani vitapamba tukio hilo la kimataifa
litakalozinduliwa jijini Dar es Salaam April 21 kabla ya kuhamia mikoani.
Pamoja na
shauku hiyo kwa wapenzi wa mashabiki wa muziki wa injili kote nchini, kwa wale
wa jijini Dar es Salaam, kumekuwa na mabadiliko ya uwanja wa kufanyia tukio
hilo la aina yake litakalowaleta pamoja waimbaji wa kitaifa na kimataifa.
Ingawa awali,
Kamati ya Maandalizi ya Tamasha hili ilitangaza kwamba uwanja wa TTCL Kijitonyana
uliopo wilayani Kinondoni ndio ungetumika kwa kishindo cha tukio hilo kwa
jijini Dar es Salaam, lakini umekosekana kwa siku hiyo.
Akizungumza
jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha hilo,
Alex Msama alisema ni kweli walipenda sana tukio hilo lifanyike hapo, lakini
wamiliki wake wamesema kwa siku hiyo ya April 21, haitawezekana.
“Kweli
tulipenda sana Tamasha la mwaka huu, lingefanyika katika Uwanja wa TCCL Kijitonyama
kutokana na kufikia vigezo tulivyotaka, lakini sasa tumeukosa kwa sababu
wenyewe wamesema siku hiyo kutakuwa na shughuli nyingine,” alisema Msama.
Akionyesha
kusikitishwa na hali hiyo, Msama alisema kwa sasa kamati yake inaendelea
kutafuta eneo jingine ambalo watafanyia tukio hilo na kudokeza tayari wanayafikiria maeneo mawili ambapo wanaendelea
na mazungumzo.
Msama
alisema, pamoja na kujitokeza kwa hali hiyo, azma ya kufanya tamasha hilo
jijini Dar es Salaam, bado ipo hasa kutokana na wadau wa jiji hilo kuukosa
uhondo wa tamasha hilo kwa miaka mitatu.
“Wadau wetu
wa muziki wa injili wa jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake, wameikosa
uhondo wa Tamasha la Pasaka kwa miaka mitatu kutokana na kufanyika mikoani
pekee, hivyo tusingependa walikose kwa mara nyingine,” alisema Msama.
Kuhusu
waimbaji, Msama alisema mazungumzo na waimbaji yapo katika hatua za mwisho na
kuanzia wiki ijayo, wapenzi na wadau wa muziki wa injili wataanza kuwajua watakaobeba
tamasha hilo.
Msama
alidokeza kuwa, kigezo kikubwa kilichotumiwa katika uteuzi wa waimbaji hao,
kwanza ni uwezo wa kuimba ‘live’ jukwaani kwa maana pasipo kutumia ‘CD’ hasa
kwa wale wazawa ili kuwajengea uwezo na ujasiri wawapo jukwaani.
“Unajua,
kitendo cha mwimbaji kuimba nyuma ya CD, kunawalemaza, unaweza kumuona mwimbaji
ni mzuri sana jumwaani, lakini kumbe ni kutokana na staili hiyo, lakini pale anapoimba
‘live’, huwa ni mwingine kabisa,” alisema Msama.
Msama
alisema kuwa, ingawa mfumo huo unaweza usiwe rafiki sana kwa baadhi ya waimbaji
kuona kama wanakomolewa, lakini unawajengea uwezo na hali ya kujiamini kuimba ‘live’
jukwaani hata wanapoalikwa kwenda nje ya Tanzania.
Kwa upande
wa malengo, Msama alisema kuwa mbali ya malengo ya msingi ambayo ni kueneza
Neno la Mungu na kutumia sehemu ya mapato kufariji makundi maalumu, safari hii
tukio hilo litabeba ajenda nyingine mahsusi.
Msama
alizitaja ajenda hizo ni kuhimiza amani na umoja wa kitaifa kwa kutambua kuwa
huo ndio msingi wa maendeleo, kwa upande wa kijamii, kiuchumi pamoja na
kisiasa.
“Mbali ya maudhui
ya jumla, mwaka huu tutakuwa na ajenda nyingine za ziada kama kuhimiza amani
hasa kwa kuzingatia kuwa, nchi itaingia katika chaguzi za serikali za Mtaa,
hivyo hali ya amani inapaswa kutamalaki,” alisema Msama.
No comments:
Post a Comment