Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akijadili jambo na Waziri wa
Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Profesa Joyce Ndalichako wakati
alipozungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo kwenye
ukumbi wa Halmashauri hiyo, Februari 19, 2019. (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu).
Baadhi ya
watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Kibondo wakimsikiliza Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza nao kwenye ukumbi wa
Halmashauri ya wilaya ya Kibondo, Februari 19, 2019.
Baadhi ya
watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Kibondo wakimsikiliza Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza nao kwenye ukumbi wa
Halmashauri ya wilaya ya Kibondo, Februari 19, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na watumishi wa
Halmashauri ya wilaya ya Kibondo kwenye ukumbi wa Halmashauri hiyo,
Februari 19, 2019. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali
Mstaafu, Emmanuel Maganga.
KIBONDO, KIGOMA
WAZIRI
Mkuu Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mweka Hazina wa Halmashauri ya
wilaya ya Kibondo, Thomas Chogolo ili kupisha uchunguzi wa
tuhuma zinazomkabili za ubadhilifu wa makusanyo ya mapato ya
halmashauri hiyo.
Pia,
Waziri Mkuu amewataka watendaji wa halmashauri huyo kumaliza haraka
migogoro yao ya kiutendaji kabla ya Serikali haijawachukulia hatua kwani
wanachokifanya ni kinyume na maelekezo yake.
Waziri
Mkuu amechukua hatua hiyo leo (Jumanne, Februari 19, 2019) wakati
akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo kwenye
ukumbi wa halmashauri hiyo akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Kigoma.
“Katika
Serikali hii suala la ukusanyaji wa mapato ni jambo nyeti na limepewa
kipaumbele, hivyo ni lazima fedha inayokusanywa itumike kama
ilivyokusudiwa ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa miradi ya maendeleo kwa
wananchi.”
Waziri
Mkuu amesema wananchi wa halmashauri hiyo wanalipa kodi kupitia kwa
watendaji wa kata katika maeneo yao lakini Mweka Hazina haingizi kwenye
mfumo wa Serikali. “Jambo hili halivumiliki.”
Amesema
mbali na fedha za makusanyo ya kodi pia matumizi ya fedha mbalimbali
zinazopelekwa na Serikali katika halmashauri hiyo nayo hayaridhizishi.
Ametoa mfano wa fedha za sekta ya Afya ambapo zaidi ya bilioni mbili
zimepelekwa na dawa hakuna.
Waziri
Mkuu amesema uaminifu na uadilifu ni jambo ambalo linapaswa kupewa
kipaumbele na watumishi wa umma, hivyo amewataka watumishi hao
wasijiingize kwenye mambo ambayo hayana tija katika utumishi wao.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu amesema Serikali imewapa dhamana watumishi hao kwa
ajili ya kuwatumikia wananchi na si kutanguliza maslahi yao binafsi,
amewataka wajirekebishe kwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
“Serikali
haitawapa nafasi ya kuendeleza migogoro yenu kila mmoja lazima atambue
majukumu yake na kuyatekeleza. Serikali haiitaji mtumishi mvivu,
masiyekuwa muadilifu na wala anayejihusisha na vitendo vya rushwa.”
Amesema
ni lazima wakamaliza migogoro ya kiutendaji ambayo imesababisha
watendaji wa halmashauri kutoelewana na kugawanyika katika makundi na
kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, FEBRUARI 19, 2019.
No comments:
Post a Comment