Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary
Mwanjelwa (Mb) akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe na Halmashauri
ya Mji wa Korogwe, wakati wa kikao kazi na watumishi hao chenye lengo la kuhimiza
uwajibikaji kwa watumishi hao kabla ya
kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF Halmashauri hizo. (Picha na Ofisi ya Rais-Utumishi).
Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary
Mwanjelwa (Mb) akiteta jambo na Katibu Tawala Mkoa wa Tanga, Bi. Zena Said,
kabla ya kuzungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe na Halmashauri
ya Mji ya Korogwe kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao kabla ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF Halmashauri
hizo.
Baadhi ya watumishi
wa umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe na Halmashauri ya Mji ya Korogwe wakimsikiliza
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) (hayupo pichani), wakati wa kikao kazi chenye lengo
la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao.
KOROGWE, TANGA
Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary
Mwanjelwa (Mb) ametoa onyo kali kwa Mweka Hazina wa Halmashauri ya Wilaya ya
Korogwe, Bw. Issai Mbilu ambaye ni Mkuu wa Idara ya Fedha na Biashara wa
Halmashauri hiyo kwa kutotekeleza majukumu yake ipasavyo na kumtaka kuacha
kiburi na kujirekebisha mara moja ili atekeleze majukumu yake kwa kutenda haki.
Onyo hilo
amelitoa wilayani Korogwe wakati wa kikao kazi na watumishi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Korogwe na Halmashauri ya Mji wa Korogwe chenye lengo la kuhimiza
uwajibikaji, kabla ya kutembelea wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ili
kukagua miradi ya TASAF na kujiridhisha na utekelezaji wake.
Mhe. Dkt. Mwanjelwa
amemtaka Mweka Hazina huyo, kutokuwa kikwazo kwenye malipo halali ya watumishi
wenzie pamoja na kutoa sababu zenye mashiko za kukataa kuidhinisha malipo ya
watumishi kwa maandishi pindi anapobaini mapungufu.
Mhe. Dkt.
Mwanjelwa amemsisitiza Mweka Hazina huyo kuacha kuipendelea idara yake katika
kulipa stahili mbalimbali ikiwamo posho ya saa za ziada kazini na kuongeza kuwa
malipo ya posho hiyo sio kwa ajili ya watumishi wa Idara ya Fedha na Biashara
pekee bali ni kwa ajili ya watumishi wote wa halmashauri kwani ni haki kwa mtumishi
yeyote aliyefanya kazi katika muda wa ziada kulipwa stahili yake.
Mhe. Dkt.
Mwanjelwa amefafanua kwamba, kitendo cha
kuwalipa posho ya saa za ziada watumishi wa Idara ya Fedha na Biashara pekee
kinashusha morali ya utendaji kazi kwa watumishi wengine.
Aidha, Mhe.
Dkt. Mwanjelwa amewataka watumishi wa halmashauri hizo kutofanya udanganyifu
ili wapate malipo yasiyostahili kwani ni kosa kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu
za utumishi wa umma na kusisitiza kuwa kila mtumishi afanye kazi kwa bidii ili
alipwe anachostahili.
Mhe.
Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) ametoa onyo kwa mtumishi huyo ili ajirekebishe, ikiwa
ni pamoja na kutoa somo kwa watumishi wote wa umma nchini wanaofanya kazi bila
kuzingatia maadili ya Utumishi wa Umma.
Dkt. Mary
Mwanjelwa (Mb) anaendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Tanga yenye lengo la
kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi kwa umma,
ikiwa ni pamoja na kukagua na kujiridhisha na utekelezaji wa miradi ya TASAF
mkoani humo.
No comments:
Post a Comment