WAZIRI
Mkuu Kassim Majaliwa ametoa siku 16 kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Rombo, Magreth John awe amepeleka asilimia 20 sawa na sh
milioni 114 ya kijiji cha Holili kabla ya Machi 10 mwaka huu, fedha hizo
zinatokana na mauzo ya madini ya pozolana.
Ametoa
maagizo hayo leo (Jumamosi, Februari 23, 2019) wakati akizungumza na
watumishi wa Kituo cha Pamoja cha Forodha cha Holili pamoja na wananchi
wa kijiji cha Holili, akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani
Kilimanjaro. Kituo hicho kipo katika mpaka wa Tanzania na Kenya.
Waziri
Mkuu alitoa maagizo hayo baada ya wananchi wa kijiji cha Holili
kuwasilisha malalamiko yao kupitia mabango wakimuomba awasaidie ili
Halmashauri hiyo iweze kulipa fedha zao zinazotokana na mapato ya mauzo
ya madini hayo yanayochimbwa kijijini kwao.
“Mkuu
wa wilaya (Agness Hokororo) simamia kuhakikisha kiasi hicho cha fedha
kinakwenda kwa wananchi na Mkuu wa Mkoa (Dkt. Anna Mgwira) nataka nipate
taarifa kuwa fedha hizo zimeshalipwa kwa uongozi wa kijiji husika.”
Kadhalika,
Waziri Mkuu amewataka watendaji katika maeneo mbalimbali nchini kuwa
wamepelekwa huko kwa ajili ya kuwahudumia wananchi, hivyo hawana budi
kutenga muda wa siku tatu kwa wiki na kwenda maeneo ya vijijini
kusikiliza kero zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi.
Wakati huo huo,
Waziri Mkuu amesema hali ulinzi na usalama katika mpaka huo si nzuri,
Serikali imeamua kuimarisha ulinzi kwenye mpaka huo, hivyo ni muhimu kwa
wananchi washirikiane katika kuulinda mpaka huo.
Hivyo,
Waziri Mkuu ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuwakamata na
kuwachukulia hatua watu wote watakaokamatwa wakipita au kuingiza mizigo
kupitia njia zisizo rasmi kwa sababu hao ndio wanaopitisha silaha.
Waziri
Mkuu amesema wananchi wa Tanzania na Kenya hawajazuiwa kufanya biashara
upande wowote bali wanatakiwa wafuate sheria, kanuni na taratibu
zilizopo katika nchi husika ikiwa ni pamoja na kutumia njia rasmi.
Amewataka
viongozi na watendaji waliopo maeneo ya mipaka huo wa Holili wawe
makini kwa sababu mpaka huo hauko salama na kuna mambo mengi
yanayoendelea ambayo yapo kinyume cha sheria.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, FEBRUARI 23, 2019.
No comments:
Post a Comment