HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 01, 2019

SIMBA; Wasahau kutufunga, tunacheza kushinda tu

NA JOHN MARWA
HATULI kushiba tunakula kumaliza, huu ni miongoni mwa misemo maarufu kaskazini mwa Tanzania hasa jijini Arusha.
Wakiwa na maana ya kuwa wanapokula hawali ili washibe bali wanakula kumaliza kilichoandaliwa kuliwa,  kilichopo mbele yao.
Hivyo ndivyo unaweza kutafsiri kauli ya Kocha Mkuu wa Simba SC Patrick Aussems, aliyoitoa baada ya kuwachana Mbao FC kwa mabao matatu mtungi juzi mjini Morogoro mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara TPL 2018/19.
Simba walishuka kwenye mtanange huo wakihitaji matokeo chanaya huku wakiwa na hasira za kulipa kisasi cha kutunguliwa na wabishi hao wa jijini Mwanza katika mchezo wa ungwe ya kwanza ya msimu huu.
Kipigo hicho kiliacha makovu ndani ya kikosi cha wekundu wa msimbazi septemba 20 2018, baada mchezo huo kumalizika Aussems na vijana wake walirushiwa chupa za maji kutoka kwa mashabiki katika Uwanja wa Kirumba walipolala 1-0.
Kinabaki kuwa kipigo pekee walichokipokea Mabingwa hao watetezi msimu huu baada ya kucheza michezo 22, sare tatu na kupoteza mmoja.
Ushindi wa juzi dhidi ya Mbao unakuwa wa 18 msimu huu, nafasi ya tatu pointi 57 nyuma ya vinara Yanga SC walioko kileleni na pointi 67 za michezo 28, nafasi ya pili Azam FC pointi 59 mechi 28.
Lilikuwa pambano la kwanza kwa Mnyama kuchezea Dimba la Jamhuri Morogoro kama Uwanja wao wa nyumbani baada ya kupisha maboresho ya Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaama kwa ajili ya maandalizi ya fainali za michuano ya AFCON kwa vijana chini ya miaka 17.
 Katika kabumbu hilo la juzi lilikuwa la ushindani wa aina yake huku Wabishi Mbao walionekanaa kuukamia mchezo, plani zao zilifeli kutokana na utulivu wa nyota wa Simba walionza katika mtanange huo.
Washambuliaji wawili John Bocco ,Adebayor,  na Meddie Kagere ,MK14, waalizitikisa nyavu na kuzichana Mbao kunako dakika za 24, 58 na 79.
Baada ya dakika 90 za kandanda hilo kumalizika Aussems alisema kila mechi wanacheza kushinda na katika mtanange huo walistahili kushinda kutokana na soka walilotandaza.
Alisema mchezo ulikuwa mgumu lakini nafasi nyingi walizotengeneza zilipelekea kuibuka na ushindi kwani walishambulia tangu mwanzo wa mchezo.
"Kila mechi tunacheza kushinda, hata huu mchezo tulistahili kushinda, tulianza kushambulia tangu mwanzo hadi mwisho, mchezo ulikuwa mgumu lakini tulitengeneza nafasi.
"Tulistahili kupata matokeo mbele ya Mbao jana (juzi tulicheza vizuri,tulishambulia, tulimiliki mpira ndio maana tumepata matokeo ya ushindi,bado tuna kazi ngumu kwa wachezaji wangu kuendelea kupambana kwa ajili ya michezo inayofuata,"alisema Aussems na kuongeza kuwa.

"Nina Imani na mashabiki wa Simba watakuwa na furaha kutokana na matokeo yetu hilo ni jambo la kujivunia, wachezaji wangu wanastahili pongezi na bado tutaendelea kupambana," alisema
Simba wamebakiza michezo sita kulingana na vinara wa Ligi Yanga SC ambao wanamichezo 28 huku tofauti ya pointi zikiwa ni 10 pekee, kama Simba anashinda viporo vyake vyote basi watawashusha watani wao na kukaa kileleni kwa tofauti ya pointi 8.
Lakini pia ushindi huo unawapa mzuka kuelekea kwenye kipute cha robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika April 6 watakapowaalika Miamba ya Afrika TP Mazembe kutoka Congo DR,  katika Dimba la Taifa jijini Dar es Salaam.
Ni mchezo unao subiriwa kwa hamu na mamilioni ya wapenda soka katika Bara la Afrika kuona nini Simba watakifanya kwa mabingwa hao mara tano wa michuano hiyo.
Hadi kufika hatua ya robo fainali Simba wamecheza michezo mitano katika dimba la nyumbani na wakipata matokeo kwa asilimia 100, michezo miwili hatua ya mtoano na mitatu hatua ya makundi.
Waliwachakaza Mbabane Swallows mabao 4-1, wakafata Nkana Red Devils 3-1 zikiwa mechi za awali na katika hatua ya makundi walianza na JS Saoura 3-0, Al Ahly 1-0 na kumalizia na AS Vita Club kwa mabao 2-1.
Itakuwa ni zamu ya Mazembe wazee wa Lubumbashi kukalia kiti kiekile walichokalia watangulizi wake katika ardhi ya Tanzania ni jambo la kusubiria kuona.

No comments:

Post a Comment

Pages